Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Uwekezaji, Mipango, na Utafiti wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), CPA T. Renata Ndege, amesema miradi mbalimbali ya miundombinu ya usafirishaji wa umeme inaendelea kutekelezwa kote nchini ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuuza na kununua umeme katika nchi jirani.
Akizungumza Januari 5, 2025, wakati wa semina ya wahariri na waandishi wa habari kuhusu mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu nishati, uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, CPA Ndege alieleza hatua zilizofikiwa katika miradi hiyo ya kimkakati.
Alisema mradi wa msongo wa kilovoti 400 (TAZA) kutoka Iringa – Mbeya – Tunduma (Songwe) – Sumbawanga na kuingia Zambia kupitia Tunduma unalenga kuiwezesha Tanzania kushiriki katika biashara ya umeme kupitia Soko la Pamoja la Umeme Kusini mwa Afrika (SAPP). Vilevile, mradi mwingine wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Singida – Manyara – Namanga (Arusha) hadi Isinya (Kenya) umekamilika na kuunganishwa na gridi ya Kenya, hatua inayowezesha biashara ya umeme katika Afrika Mashariki.
CPA Ndege alieleza pia maendeleo ya miradi mikubwa ya uzalishaji wa umeme, ikiwa ni pamoja na mradi wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115 ambao umefikia asilimia 99.55 ya utekelezaji, mradi wa Malagarasi Kigoma wa Megawati 49.5 ambao uko asilimia 4.8, na mradi wa sola wa Shinyanga awamu ya kwanza wa Megawati 50 ambao umefikia asilimia 38.
Aidha, TANESCO inatekeleza miradi ya uzalishaji wa umeme kupitia vyanzo mbadala kama jua, upepo, gesi, na tungamotaka, miradi ambayo iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Semina hiyo ililenga kuwajengea uelewa wahariri na waandishi wa habari kuhusu mchango wa Tanzania katika ushirikiano wa kikanda kupitia sekta ya nishati, hususan biashara ya umeme.
Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati umepangwa kufanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania, tarehe 27 na 28 Januari 2025.
Mkutano huu utahusisha wakuu wa nchi 54 za Afrika, pamoja na marais wa Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Umoja wa Afrika, mawaziri wa fedha, na wadau wengine muhimu katika sekta ya nishati.
Lengo kuu la mkutano huu ni kujadili na kuimarisha ushirikiano katika sekta ya nishati barani Afrika, ikiwa ni pamoja na kusaini Mpango wa Nishati ambao ni ahadi ya pamoja ya nchi 14 katika kukuza na kuboresha upatikanaji wa nishati safi na endelevu.
Mkutano huu ni matokeo ya juhudi za viongozi wa Afrika katika kuhakikisha upatikanaji wa nishati bora kwa maendeleo endelevu ya bara hili.