Na Sophia Kingimali.
Mkuu wa Chuo cha Furahika kilicho chini ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Dkt. David Msuya ametoa rai kwa wakuu wa vyuo vyote nchini kuwa na Walimu wanaofundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu huku akiomba miundombinu ya vyuo hivyo iwe rafiki kwa watu hao.
Wito huo ameutoa leo Januari 6,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Amesema ili kuzingatia utawala bora na haki ya kusoma ya kila mtanzania miundombinu ya mahali pa kutoa elimu inatakiwa ifikike kwa kila mmoja.
“Msiweke madarasa yenye ngazi kwaajili ya watu wenye ulemavu hasa ya wale wanaotambaa au wanaotembea kwa njia ya baiskeli, wanashindwa kuingia darasani kwa sababu ya madarasa mengi yamekuwa na ngazi” Amesema Dkt. Msuya
Aidha ameongeza kuwa serikali na taasisi nyingine zinapoandaa miradi ya elimu inapaswa kuzingatia kujenga miundombinu itakayowawezesha watu wenye mahitaji maalum kuweza kuitumia.
Amesema kuwa vyuo vinapaswa kuwa na walimu wa lugha za alama ili kuwatendea haki watu wenye ulemavu kwenye vyuo na kuwafanya watu wenye mahitaji maalum wote kupata elimu sawa na wanafunzi wengine ambao hawana ulemavu.
“Niipongeze wizara ya elimu imejitahidi sana kwani inayowalimu wengi wanaofundisha lugha za alama, 2025 Vyuo tubadilike tutafute walimu, wawepo kila idara ili tutimize ndoto za serikali za awamu ya sita kupitia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani, nia yake ni njema sana lakini taasisi hizi za elimu tunatakiwa tujiongeze sisi wenyewe kuona kwamba tunawainua watu wenye mahitaji maalumu.” Amesema
Amesema kuwa Chuo Chake wamefanikiwa kupata walimu wa watu wenye mahitaji wawili, pia amewaomba vyuo vingine walifanye jambo hilo ili watanzania wenye mahitaji wawe na haki sawa kama walivyo wengine kwa kupata elimu na ujuzi.
Aidha ameongeza kuwa kuanzia Aprili, 2025 chuo hicho kinatarajia kuanzisha fani ya ushonaji viatu pamoja na kazi ya uhudumu kwenye magari kwani kunawatu wanausafiri wa mabasi lakini hakuna wahudumu.
“Kuna watu wenye uhitaji wengi wakiwemo wasioona ambao wamekuwa na ujuzi mbalimbali ikiwemo ufundi na utengenezaji wa viatu hivyo kama chuo tumejipanga kuhakikisha tunatoa elimu hiyo kwa hao wahitaji”,Amesema.
“Ulemavu unaweza kumkuta mtu yeyote kwahiyo soko la ajira lisichague ili kila mmoja anufaike na miradi mbalimbali inayoanzishwa na serikali.” Amesema Dkt. Msuya.
“Ili kupunguza ukatili na tutende haki pande zote mbili tutende haki kwa walemavu wa mikono, wa miguu, macho na wasio sikia kwani Wanahaki ya kupata mafunzo ya veta ili watimize malengo yao na tujiongeze kubadilishana ujuzi kutoka vyuo tofauti tofauti ndani na nje ya nchi.” Amesema Dkt. Msuya
Licha ya hayo Dkt. Msuya pia amewakaribisha Watoto wote waliopo mtaani, waliofeli darasa la Saba na kidato cha nne kuanzia mwaka 2022 mpaka sasa kujiunga na chuo hicho kwani mpaka sasa kinanafasi 400 za kujiunga.
Ameongeza kuwa fomu za usajili zinapatikana katika tovuti ya chuo hicho ya www.furahika.co.tz.