Katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2024, Serikali ya Tanzania imefanikiwa kufikisha umeme katika vijiji 12,278, sawa na asilimia 99.7 ya vijiji vyote nchini. Aidha, vitongoji 32,827 vimefikiwa na umeme kati ya vitongoji 64,359, sawa na asilimia 51. Hatua hii imeongeza fursa kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kuboresha sekta muhimu kama elimu, afya, biashara, na usafiri. Kwa mujibu wa takwimu, zaidi ya taasisi za afya na elimu 12,905 zimeunganishwa na umeme, hatua ambayo imeimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Zaidi ya hayo, Serikali imewekeza katika vyanzo mbadala vya nishati kama umeme jua, jotoardhi, na upepo, ambapo uzalishaji unatarajiwa kuongezeka kwa megawati 1,100. Hii inalenga kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta ya viwanda, ambapo idadi ya viwanda vya uzalishaji wa vifaa vya nishati kama nguzo na nyaya imeongezeka kutoka 23 mwaka 2020 hadi kufikia viwanda 78 mwaka 2024. Uzalishaji wa ndani wa vifaa hivi siyo tu unatoa ajira kwa Watanzania, bali pia unapunguza gharama za usambazaji wa nishati vijijini na mijini.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, wakati akifungua semina ya wahariri wa vyombo vya habari na waandishi wa habari kuhusu Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati. Semina hiyo imefanyika katika ukumbi wa Maktaba, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, leo Januari 5, 2024.
Mkutano huo, ambao unatarajiwa kufanyika Januari 27-28, 2025, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, ni matokeo ya juhudi kubwa za kidiplomasia za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Rais Samia ameonyesha uongozi wa mfano barani Afrika kwa kusimamia ajenda ya nishati safi ya kupikia, ambapo kupitia Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi wa mwaka 2024-2034, Tanzania imelenga kufikia asilimia 80 ya kaya kutumia nishati safi ifikapo mwaka 2034. Hatua hii inalenga kuboresha afya za wananchi na kulinda mazingira dhidi ya uharibifu wa misitu unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa.
Bw. Msigwa alisisitiza kwamba mkutano huo utaweka msingi wa kupatikana kwa umeme kwa Waafrika milioni 300, ambapo nchi 14 za Afrika zitatia saini makubaliano hayo mbele ya marais zaidi ya 10 wa Afrika. Pia, amewataka waandishi wa habari kushirikiana kwa dhati na Serikali kufanikisha mkutano huo, huku akibainisha kwamba Tanzania inayo nafasi ya kipekee kuimarisha taswira yake kimataifa kupitia tukio hili.
“Ndugu wahariri na waandishi wa habari, nyinyi ni daraja muhimu kati ya Serikali na wananchi. Hakikisheni taarifa sahihi kuhusu juhudi za Serikali zinawafikia wananchi. Kupitia mkutano huu, tunawataka kuelewa kwa undani ajenda zake na kuelimisha umma kuhusu umuhimu wake,” alisema Bw. Msigwa. Alimalizia kwa kutoa wito wa kuweka ajenda moja ya kuijenga taswira chanya ya Tanzania kimataifa, akisisitiza kwamba “Tanzania Kwanza!”