Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula ametoa msaada wa vyakula ikiwemo Mchele na Sukari kwa wananchi wa mitaa ya Butindo kata ya Shibula kaya13, Kilabela kata ya Bugogwa kaya 12 na Isanzu kata ya Sangabuye kaya 2 kufuatia maafa ya mvua kubwa zilizoambatana na upepo zilizonyeesha usiku wa kuamkia Januari 02, 2025
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo Katibu wa Mbunge Ndugu Charles David Karoli amesema kuwa mbunge anatoa pole nyingi kufuatia madhara ya mvua hizo ikiwemo kunyeshewa kwa vyakula vilivyokuwa vimehifadhiwa majumbani
‘.. Wakati mvua zinanyesha na kuezua mapaa ya nyumba ndani kulikuwa na vyakula, Na baadhi yenu mkajikuta vyakula vimenyeeshewa hivyo Mbunge akaona ipo haya ya kutoa msaada wa vyakula kwa wakati huu wakati tukisubiria hatua nyengine zitakazochukuliwa na Serikali ..’ Alisema.
Aidha Mbunge Dkt Mabula amewashauri wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya mvua zinazoendelea kunyesha ili kujikinga na madhara mengine yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua zinazoendelea maeneo mbalimbali nchini sanjari na kuwapongeza viongozi wa mitaa na kata kwa namna walivyoshirikiana katika kusaidia wananchi waliopatwa na majanga hayo.
Swila Dede ni diwani wa kata ya Shibula moja ya eneo lililoathiriwa na mvua hizo ambapo amemshukuru Mbunge Dkt Angeline Mabula kwa msaada alioutoa huku akiwataka wananchi wake kumuunga mkono Mbunge huyo na kuwapuuza watu wasiokuwa na nia njema wanaotumia matatizo yao kama sehemu ya mtaji wa kisiasa na kujinufaisha wao binafsi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Butindo ndugu Lucas Andrea amempongeza Mbunge Dkt Angeline Mabula na kwamba wanamuombea Mungu amzidishie pale alipopunguza huku akiwaasa wananchi wake kushirikiana wakati wa kipindi hiki kigumu.
Samuel Miza ni miongoni mwa wananchi waliokumbwa na maafa hayo ambapo amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Ilemela huku akiwaasa viongozi wengine kuiga mfano huo.
Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula pia ameagiza kufanyika kwa tathimini fupi juu ya madhara ya mvua hizo kwa wananchi wote walioguswa na kadhia ili kutoa fursa kwa Serikali kuchukua hatua zaidi kwa kushirikiana na ofisi yake.