Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari, akizungumza na waombolezaji na Watanzania leo, Januari 2, 2025, wakati aliposhiriki tukio la kuaga mwili wa Mwanasheria Mkuu Mstaafu, Jaji Fredrick Werema kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari, akiaga mwili wa Mwanasheria Mkuu Mstaafu, Jaji Fredrick Werema leo, Januari 2, 2025, wakati aliposhiriki tukio hilo katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
…………….
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari, ameungana na Watanzania leo, Januari 2, 2025, kuaga mwili wa Mwanasheria Mkuu Mstaafu, Jaji Fredrick Werema, katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam. Katika hotuba yake, Mhe. Johari amemkumbuka marehemu kwa utendaji wake bora, kujitolea kwa dhati, na kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha sheria na haki zinatumika kuleta maendeleo ya Taifa.
Mhe. Johari amesema kuwa marehemu Jaji Werema, wakati wa uhai wake, alihudumu katika Wizara na taasisi mbalimbali za serikali, ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Ameeleza kuwa kifo chake ni pigo kubwa, hususan kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwani alikuwa kiongozi mwenye maono na mtaalamu wa sheria aliyejitolea kwa dhati katika kuimarisha utawala wa sheria nchini.
Akielezea safari ya kikazi ya Jaji Fredrick Werema, Mhe. Johari amesema kuwa mnamo Aprili 1, 1984, marehemu aliajiriwa kama Wakili wa Serikali katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kupanda madaraja hadi kufikia nafasi ya Wakili wa Serikali Mkuu.
Mwaka 1993, akiwa Wakili wa Serikali Mkuu, aliongoza majadiliano katika mikataba ya kimataifa ya biashara ya Umoja wa Mataifa na kusimamia mashauri mbalimbali ya serikali kwa kuiwakilisha Tanzania.
Mwaka 1998, aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Katiba na Haki za Binadamu katika Wizara ya Katiba na Sheria. Katika nafasi hiyo, aliwezesha kuanzishwa kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Tume ya Uchaguzi, na kuratibu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini.
Kati ya mwaka 2005 na 2009, marehemu alifanya kazi kama Jaji katika mahakama za ndani na nje ya nchi, ambapo alitoa maamuzi muhimu katika mashauri ya kibiashara na mikataba, yenye mchango mkubwa katika kukuza biashara na uchumi wa Taifa.
Kuanzia Oktoba 2009 hadi 2014, aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, nafasi aliyoitumia kufanya maboresho ya mifumo ya sheria, kuimarisha utawala wa kisheria, na kuendeleza wanasheria nchini.
Mhe. Johari amesema kuwa marehemu Jaji Werema ameacha alama isiyofutika katika sekta ya sheria na haki za binadamu. Marehemu alifariki dunia Desemba 30, 2024, na ataendelea kukumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Taifa.
Mwili wa marehemu unatarajiwa kuzikwa siku ya kesho katika makaburi ya familia huko mkoani Mara.
Rais mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungunza katika na waombolezaji.
Jaji mkuu mstaafu Jaji Mohammed Othman Chande akiaga mwili wa jaji Fredrick Werema.
Mwanasheria mkuu wa serikali mstaafu Mhe. Andrew Chenge akiaga mwili wa marehemu Fredrick Werema.
Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Ally Possi akiaga mwili wa Marehemu Jaji Fredrick Werema.