Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula amewafariji wananchi wa mtaa wa Butindo kata ya Shibula na Kilabela kata ya Bugogwa kufuatia maafa yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha usiku wa kuamkia Jumatano ya Januari 02, 2025
Akizungumza na wananchi waliokumbwa na kadhia hiyo kwa niaba ya Mbunge, Katibu wa Mbunge Ndugu Charles David Karoli amesema kuwa Mhe Mbunge amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za madhara ya mvua zilizotokea usiku wa kuamkia Leo na kwamba anazipa pole kaya 13 zilizoathirika na mvua hiyo huku tathimini ya awali ikionesha athari kubwa iliyopatikana ni uharibifu wa vyakula, kuezuliwa kwa mapaa ya nyumba na watu wawili kujeruhiwa kichwani kwa kuangukiwa na matofali na mbao
‘.. Mbunge ameipongeza Serikali kwa juhudi za haraka ilizozichukia katika kukabiliana na maafa haya lakini pia Kamati zetu za nzengo zinazosimamia maafa kwa kusaidia wenzetu na kuwafariji wakati tukisubiria misaada ya wadau wengine ..’ Alisema
Aidha Ndugu David akaongeza kuwa Mbunge ataendelea kufanya jitihada mbalimbali kuhakikisha wananchi waliopata madhara wanasaidiwa huku akiwaasa kuchukua tahadhari kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Butindo ndugu Lucas Andrea amefafanua kuwa mvua iliyoleta madhara ilikuwa imeambatana na upepo mkali pamoja na vidonge vya theluji za barafu na kwamba kama mtaa wameshatoa kiasi cha fedha kusaidia wananchi katika kukabiliana na maafa ya mvua hizo sanjari na kuwaandalia maeneo ya kujistiri kwa siku kadhaa wakati wakisubiria kurejea kwa hali za maisha ya kawaida ya kila siku.
Paschal Mahiba ni Katibu wa CCM kata ya Shibula ambapo amempongeza na kumshukuru Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kwa kuchukua hatua za haraka katika kuwafariji wananchi waliopatwa na maafa ya mvua huku akiwaasa wananchi wa kata hiyo kuendelea kushirikiana nae katika shughuli za kila siku za maendeleo
Nae Samuel Miza Kayenze ambae ni Moja ya wananchi waliokumbwa na maafa hayo mbali na kumshukuru Mbunge Dkt Angeline Mabula amewataka viongozi wengine kuiga mfano wake kwani amekuwa akijitoa kwa hali na mali na kwa wakati pindi wananchi wake wanapokubwa na majanga mbalimbali