Mwakilishi wa Mwenyekiti wa tume huru ya taifa ya uchaguzi INEC Adam Mkina
Baadhi ya wadau walioshiriki katika mkutano wa tume huru ya taifa ya uchaguzi
Picha ya pamoja na machifu waliohudhuria katika mkutano huo
Katika picha ya pamoja na viongozi wa siasa walioshiriki katika mkutano huo
Kaimu mkurugenzi wa tume huru ya taifa ya uchaguzi Martin Mnyenyelwa wakati akitoa wasilisho mbele ya mgeni rasmi
Katikati ni mwakilishi wa Mwenyekiti wa Tume huru ya taifa ya uchaguzi Adam Juma Mkina.picha na Neema Mtuka.
………………….
Na Neema Mtuka Sumbawanga
Rukwa:
Tume huru ya taifa ya uchaguzi (INEC) imewataka viongozi wa vyama vya siasa kuzingatia taratibu kanuni miongozo na sheria katika kipindi chote cha uandikishaji na uboreshaji wa taarifa za wapiga kura katika daftari la kudumu la wapiga kura.
Hayo yamesemwa leo Desemba 31,2024 na Mwenyekiti wa tume huru ya taifa ya uchaguzi (INEC) Jaji Jacob Mwambegele akiwakilishwa na kaimu mwenyekiti Adam Juma Mkina wakati wa mkutano wa tume huru ya taifa ya uchaguzi na wadau kuhusu uboreshwaji wa daftari la kudumu la wapiga kura katika ukumbi wa mikutano manispaa ya Sumbawanga.
Mwambegele amesema viongozi wa siasa wanapaswa kutoa mawakala kwa ajili ya kuangalizi kwa kuwa wao wanafahamiana na ni rahisi kutambua mtu asiye na sifa ya kujiandikisha.
Amewahimiza wananchi kujitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao na kuacha tabia ya kutoa taarifa za uongo na endapo watabainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Sambamba na hilo pia amelitaka jeshi la polisi kuhakikisha linaimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao na hasa vifaa vitakavyotumika katika zoezi hilo.
Aidha amewasisitiza viongozi wa dini kutumia nyumba za ibada kuwaelimisha waumini wao na kuwahamasisha kujitokeza katika uboreshaji wa taarifa katika daftari la kudumu la wapiga kura.
“Tumieni madhabahu zenu kuwaelimisha waumini wenu na sio kuhubiri kuhusu chama fulani cha siasa na badalà yake hamasa iwe kubwa kwa wananchi kujitokeza kujiandikisha.
Awali akitoa wasilisho mbele ya mgeni rasmi kaimu mkurugenzi wa tume huru ya taifa ya uchaguzi Martin Mnyenyelwa amesema wapiga kura ni lazima wakidhi vigezo vya mpiga kura katika zoezi la uandikishaji.
Kwa upande wake mwakilishi wa idara ya (TEHAMA ) Innocent Cosmas amesema mfumo utakaotumika kujiandikisha VRS umefanyiwa maboresho makubwa kwa kuunganishwa na NIDA ili kulifanya zoezi hilo kuwa rahisi.
Naye chief Kapele wa ufipa amesema wanaishukuru Tume huru ya taifa ya uchaguzi kwa kuwashirikisha katika mkutano huo na kuahidi kuwahamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha.
“Tutahamasisha wananchi kujitokeza na kujiandikisha na kuwahimiza kuachana na dhana potofu ya kuwa hata tusipopiga kura watapita wale wale wa chama fulani”amesema chifu.
Nao baadhi ya viongozi wa dini akiwemo mchungaji Daniel Mwakyoma amesema watahakikisha wanawahamasisha waumini wao kwani kupiga kura ni haki ya kila raia.
Mkoa wa Rukwa una halmashauri 4 majimbo 5 kata 97 na vituo 734 ikiwa ni ongezeko la vituo 30 ikilinganishwa na vituo 704 vilivyotumika kuandikisha wapiga kura katika mwaka 2020.
Kwa mujibu wa takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 baada ya kukamilika kwa zoezi hilo mkoa wa Rukwa unatarajia kuwa na wapiga kura 753,229 ikiwa ni ongezeko la wapiga kura 114,250 ikilinganishwa na wapiga kura 638,979 waliopo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura walioandikishwa kwa mwaka 2020.
Mkutano huo umebeba kauli mbiu ya Isemayo “Kujiandikisha kwa mpiga kura ni msingi wa uchaguzi bora”.