Wakazi wa vijiji vinavyozunguka Pori la akiba la Grumeti katika wilaya za Bunda na Serengeti mkoani Mara wameiomba serikali kuja na mbinu mbadala ya kukabiliana na wanyama waharibifu wa mashamba na mazao hasa tembo kutokana na ongezeko la matukio ya wanyama hao kuvamia vijiji hivyo kwa lengo la kula mazao mashambani.
Wamesema licha ya jitihada zinazofanywa na Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Grumeti Fund ya kutoa mafunzo ya kuzuia wanyama hao, hivi sasa kumekuwepo na ongezeko kubwa la matukio ya wanyama hao kuvamia vijiji hivyo na kujaribu kuharibu mazao shambani jambo ambalo linapaswa kutafutiwa ufumbuzi wa haraka kabla hali haijawa mbaya.
Hata hivyo wamesema licha ya uwepo wa uvamizi huo mkubwa unaotokana na ongezeko la wanyama hao lakini uharibifu wa mashamba na mazao umepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na mafunzo waliyoyapata juu ya namna ya kukabiliana na wanyama hao kutoka kwa taasisi hiyo ya Grumeti fund pale tembo wanapovamia vijiji hivyo.
Uharibifu huo umepungua kutokam atukio ya kila siku hadi tukio moja kwa mwezi kutokana na uwepo wa vikundi hivyo vya kufukuza tembo ambavyo vimepewa mafunzo namna ya kukabiliana na wanyama hao hatua ambayo imekuwa ikipelekea wawe na uwezo wa kuwafukuza wanayama hao pale wanapovamia vijiji hivyo kabla ya kufanya uharibifu kwenye mashamba na mazao.
Wakizungumza katika kijiji cha Mariwanda wilayani Bunda leo Desemba 29,2024 wakati wa mafunzo juu ya namna ya kutoa huduma ya kwanza yaliyokwenda sambamba na ugawaji wa vifaa vya huduma baadhi ya wakazi hao wamesema kabla ya kupata mafunzo ya namna ya kukabiliana na wanayama hao hali ya uharibifu wa mashamba na mazao yao hali iliyokuwa ikisbabisha ukosefu wa chakula cha kutosha kwa wakazi hao.
Wamesema wamebaini ipo haja ya kupata mbinu tofauti tofauti katika kukabiliana na wanyama hao kwa maelezo kuwa mbinu wanazotumia hivi sasa ikiwa ni pamoja na matumizi ya tochi na filimbi zimeanza kuzoeleka na wanyama hao tofauti na awali walipoanza kuzitumia.
“Zamani tembo ulikuwa ukimmulika na tochi alikuwa anakimbia lakini kwasasa ni kama wameanza kuzoea kwahiyo ni vema tukapata mafunzo na mbinu mbadala ambazo zinaweza kuwa suluhisho la kudumu juu ya changamoto hii,” amesema Mathias Kapeta Mkazi wa kijiji cha Hunyari
Kapeta amesema endapo hapatakuwa na mbinu mpya upo uwezekano wa uharibifu wa mashamba na mazao kuwa mkubwa kama ilivyokuwa awali hali ambayo itahatarisha usalama wa chakula katika vijiji hivyo kwa maelezo kuwa matukio ya wanyama kuvamia vijiji hivyo huinhezeka zaidi hasa nyakati za mavuno.
Mkazi wa Kijiji cha Mariwanda wilayani Bunda, Francis Kitashi amesema kipindi cha nyuma uharibifu ulikuwa mkubwa ingawa wanyama hao hawakuwa wengi kama ilivyo sasa mbapo wanyama wameongezeka hivyo kama wangekuwa hawana mafunzo basi hali ingekuwa mbaya zaidi.
“Tunashukuru kwa namna ambavyo Grumeti wamekuwa wakitusaidia ila tunaomba kupewa mbinu zaidi, kwani wanyama hawa wamenza kuzoea mbinu tunazotumia lakini pia wameongezeka sana” amesema Maswi Thobias mkazi wa kijiji cha Mihale wilayani Bunda
Kuhusu mafunzo na vifaa vya kutolea huduma ya kwanza wakazi hao wamesema kulikuwa na uhitaji mkubwa kutokana na baadhi yao kupata majeraha mara kwa mara pale wanapowafukuza tembo na wanyama wengine wanaovamia vijiji vyao.
Mkazi wa Kijiji cha Singisi wilayani Serengeti, Rashid Manota amesema mara nyingi wamekuwa wakipata majeraha na kukazimika kukaa na maumivu bila kupata huduma ya kwanza pale wanapokuqa mbali na vituo vya kutilea huduma za afya.
“Mmoja wetu alipata jeraha kubwa tukiwa tunafukuza tembo na kwavile tulikuwa mbali sana ilibidi alale usiku kucha huku akivuja damu kwasababu hatukuwa na elimu namna ya kumpa huduma ya kwanza yaani hadi anafikishwa hospitalini kesho yake tayari alikuwa amepoteza damu nyingi, hivyo mafunzo haya na vifaa hivi ni muhimu sana kwetu sisi hasa tunaofanya shughuli hii ya kuwafukuza wanyama waharibifu,”amesema Manota
Mkuu wa Idara ya Mahusiano wa Taasisi ya Grumeti Fund, David Mwakipesile amesema ,taaaisi yake imeamua kutoa mafunzo ya kuzuia na wanyama pori waharibifu hususani tembo na mafunzo ya huduma ya kwanza kwa vikosi vya kufukuza wanyamapori hao kutokana na uwepo wa uvamizi wa mara kwa mara unaofanywa na wanyama hao katika vijiji hivyo.
Mwakipesile amesema mara kadhaa wakazi hao wamekuwa wakipata majeraha ambayo wakati mwingine yamekuwa yakihatarisha maisha yao pale wanapowafukuza tembo kutoka katika vijiji hivyo na kwamba kutokana na hali hiyo waliona upo umuhimu wa uwepo wa vifaa vya huduma ya kwanza pamoja na elimu ya awali juu ya namna ya kutoa huduma hiyo pale itakapokuwa inahitajika.
“Ni kweli kuna vituo vya kutolea huduma za afya maeneo mengi lakini hawa watu wamekuwa wakipata majeraha wakati mwingine wakiwa huko ndani ndani hivyo taasisi ikaona ipo haja ya kuwapa hivi vifaa ili pale tu mtu anapoapta shida aweze kupata huduma ya kwanza kunusuru uhai wake wakati wakifanya utaratibu wa kumfikisha kwenye kituo cha kutolea huduma kwa matibabu zaidi,” amesema
Amesema vifaa hivyo vimetolewa kwa vijiji 20 vinavyozunguka pori hilo huku wakiamini vitakuwa na tija hasa katika kipindi hiki ambacho kumekuwepo na ongezeko la wanyama hali inayoplekea uwepo wa ongezeko pia uvamizi wa wanyama vijijini kwa lengo la kula mazao mashambani.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Vicent Naano amesema kutokana na ongezeko hilo la wanyama kuvamia vijiji, serikali imekuwa ikifaya jithada mbalimbali kuhakikisha wanyama hao hawaleti madhara zaidi kwa binadamu.
Amesema jitihada hizo ni pamoja na ushirikiano na wadau mbalimbali ikiwemo taasisi ya Grumeti fund ambapo amesema kwa namna moja ama nyingine jitihada hizo zimeleta mafanikio ikiwa ni pamoja na kupunguza uharibifu wa mashamba na mazao ya wananchi tofauti na ilivyokuwa awali.
“Ni kweli tembo wanavamia vijiji hata juzi walikuwa kule Guta lakini madhara yamepungua kwani hawafiki kwenye mashamba tunachofanya mbali na ushirikiano na wadau kama Grumeti lakini pia idara ya wanyamapori inafanya doria saa 24 kwahiyo tukipata tu taarifa askari wanafika eneo la tukio kwa haraka na kuwarudisha tembo hifadhini,” amesema