Katika kuchochea maendeleo ya Kaya na jamii kwa ujumla, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii–TASAF unatekeleza miradi 7 ya Maendeleo yenye thamani ya Shilingi bilion 1.32 Kisiwani Pemba.
Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa miundombinu mbnalimbali katika sekta ya elimu, afya na madaraja kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii na kuwezesha jamii kuondokana na hali ya umaskini.
Hayo yamebainishwa wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Skuli ya Dodo Kisiwani Pemba inayojengwa na TASAF kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 184.8.
Jiwe la msingi na Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe.Shaaban Ali Othman katika muendelezo wa Shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Akizungumza mara baada ya kuweka jiwe la msingi, Mhe Othman aliipongeza TASAF kwa kuendelea kusaidia jamii katika kujikwamua na umaskini na kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu lenye lengo la kuinua hali ya uchumi wa kaya na jamii kwa ujumla.
“TASAF inafanya kazi kubwa sana katika kusaidia jamii na kaya za wahitaji kuimarfika kiuchumi, Kupitia utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, tunaishukuru sana kwa kuwezesha jamii na kuinua hali za wananchi wote,” alisema.
Waziri huyo aliongeza kwamba juhudi zinazofanywa na TASAF zinatakiwa kuenziwa kwa kuhakikisha miundombinu inayojengwa inalindwa na kutunzwa kwa manufaa ya kizazi kilichopo na kijacho.
“Miradi hii ni yetu sote, tusiihujumu, tusaidiane kuhakikisha inakamilika kwa wakati ili watoto wetu wasiwe wanakwenda umbali mrefu kufuata elimu, pia tuutunze ili udumu kwa muda mrefu baada ya kukamilika kwake,” aliongeza.
Akizungumza kwa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Shedrack Mziray, Mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa TASAF Bw. Peter Lwanda alisema, katika kipindi cha Pili cha Mpango imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi 15 ya kuendeleza miundombinu katika sekta ya Elimu, Afya na Maji. Miradi hiyo imegharimu zaidi ya shillingi Bilioni 3.1.
“Kwa mwaka huu wa fedha, jumla ya miradi 7 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.32 imetekelezwa katika kisiwani Pemba, miradi hiyo inahusisha sekta tofauti ikiwemo elimu ambayo miongoni mwa miradi yake ni ujenzi wa Skuli hii ya Dodo iliyowekwa jiwe la msingi leo. Miradi mingine ni ya afya pamoja na miundombinu ya ujenzi wa madaraja,” alisema.
Aliongeza kuwa TASAF imeunganisha kanzidata na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) ili kuwezesha waombaji wa mikopo ya elimu ya juu kutoka kaya za Walengwa kutambulika kirahisi na kuwa wanufaika wa Mikopo hiyo ya elimu ya juu kwa asilimia 100.
“Ushirikiano huo umeongeza idadi ya wanafunzi wanaopata mikopo kutoka kaya za walengwa ambapo jumla ya wanafunzi 8,274 wamenufaika na utaratibu huu hadi kufikia Novemba 2024 na hivyo kupunguza changamoto za watoto kutoka kaya hizo kupata nafasi za masomo katika vyuo vya elimu ya juu,” alisema.