Na Sabiha Khamis, Maelezo
Mkurugenzi Mtendaji Baraza la Mitihani la Zanzibar Dkt. Rashid Abdul-aziz Mukki amesema kwa mujibu wa matokeo ya Mtihani wa Darasa la Saba ya mwaka 2024 yanaonesha kuwa ufaulu umepanda kwa asilima 1.66 kutoka asilimia 95.00 ya mwaka 2023.
Akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari kuhusu matokeo ya mtihani wa Taifa wa darasa la Saba kwa mwaka 2024 katika ukumbi wa Wizara ya Elimu Mazizini Wilaya ya Magharib.
Amesema watahiniwa 44,486 sawa na asilimia 96.66 waliofanya mtihani wamefaulu kwa madaraja ya A, B, C, na D. Watahiniwa 1,535 sawa na asilimia 3.34 wamepata daraja la F.
Ameeleza kuwa kwa mwaka 2024 ufaulu umeengezeka katika madaraja ya C na D ambapo watahiniwa waliofaulu wanaume 20,571 sawa na 46.24% na wanawake 23,915 sawa na 53.76%, kwa watahiniwa waliopata Daraja F wamepunguwa kwa 1.66% kutoka 5.00% mwaka 2023 hadi 3.34%.
Aidha ameelezea ubora wa ufaulu ambapo watahiniwa 228 (0.50%) wamefaulu kwa wastani wa juu wa Daraja A, watahiniwa 4,816 (10.46%) wamefaulu kwa wastani wa Daraja B, pamoja na watahiniwa 20,459 (44.46%) wamefaulu kwa wastani unaoridhisha wa Daraja C, wakufuwatiwa watahiniwa 18,983 (41.25%) wamefaulu kwa wastani wa Daraja D na watahiniwa 1,535 sawa na asilimia 3.34% wamepata wastani wa chini wa Daraja F.
Amesema ufaulu wa masomo kwa ujumla katika mwaka 2024, unaonesha kuwa somo la ubunifu wa Sanaa,michezo na Sayansi jamii ni yenye ufaulu wa juu zaidi 99.68% ikilinganishwa na mwaka 2023.
Aidha, somo la lugha ya Kiswahili ufaulu wake umepanda kwa asilimia 94.87 (5.55%) ikilinganishwa na asilimia 89.32 mwaka 2023. Pia, somo la hesabati ufaulu wake umepanda kwa asilimia 55.52 (5.42%) ikilinganishwa na asilimia 50.10 ya mwaka 2023.
Amefahamisha kuwa jumla ya watahiniwa 46,948 wamesajiliwa kufanya mtihani wa Darasa la Saba mwaka 2024, kati yao wanaume ni 22,408, sawa na asilimia 47.73 na wanawake ni 24,540 sawa na asilimia 52.27, idadi hiyo imeongezeka kwa watahiniwa 2,222 sawa na asilimia 4.97 ikilinganishwa na watahiniwa 44,726 waliosajiliwa mwaka 2023 ambapo jumla ya vituo 478 vilisajiliwa, kati ya hivyo 293 vya Skuli za Serikali na 185 vya binafsi hii inaonesha kuwa ongezeko la vituo 24 sawa na asilimia 5.02 ikilinganishwa na Vituo 454 vilivyosajiliwa mwaka 2023.
Amefafanua kuwa watahiniwa 224 wenye mahitaji maalumu walisajiliwa kufanya mtihani kwa mwaka 2024 kati yao Wasioona 3, wenye uoni hafifu 74, ulemavu wa viungo 6, ulemavu mchanganyiko 5, viziwi 39 na watahiniwa wenye ulemavu wa akili 97 ambapo watahiniwa wenye mahitaji maalumu waliofanya Mtihani katika mwaka 2024 ni 217, wakiwemo wasioona 3, wenye uoni hafifu 73, ulemavu wa viungo 6, ulemavu mchanganyiko 5, viziwi 37 na watahiniwa wenye ulemavu wa akili 93.
Akielezea utoro utoro wa watahiniwa hao umepunguwa ambapo jumla ya watahiniwa 927 walisajiliwa ambao hawakufanya mtihani kwa mwaka 2024 idadi imepunguwa kwa watahiniwa 225 sawa na 19.53% ikilinganishwa watahiniwa 1,152 ambao hawakufanya mtihani mwaka 2023.
Amebainisha kuwa watahiniwa 642 kutoka vituo 25 wanatuhumiwa kufanya udanganyifu hivyo matokeo yao yamezuliwa kwa mujibu wa kifungu cha 57 (b) cha kanuni za mitihani ya Baraza la Mitihani la Zanzibar ya mwaka 2014 hadi uchunguzi utakapokamilika kwa watahiniwa ambao watapatikana na hatia watafutiwa matokeo kwa mujibu kifungu cha 6 (1) cha Sheria Nam. 6 ya mwaka 2012 ya Baraza la Mitihani la Zanzibar ikisomwa sambamba na kifungu nambari 58 (1) cha Kanuni za Mitihani za Baraza la Mitihani la Zanzibar za mwaka 2014.