TAWA yaendeleza Kasi ya kutoa elimu
Na Mwandishi wetu, Rukwa
SERIKALI imekamilisha mchakato wa kufanya tathmini ya malipo ya kifuta jasho kwa wananchi 27 wa wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa ambao mazao yao yaliathiriwa na wanyamapori wakali na waharibifu katika kipindi cha mwaka 2022 mpaka 2024
Kauli hiyo imetolewa Desemba 22, 2024 na Afisa Wanyamapori Wilaya ya Nkasi Bw. Anorld Ngagashi akiongea na wananchi wakati wa ziara ya mafunzo ya mbinu za kukabaliana na wanyamapori wakali na waharibifu hususani tembo, ziara iliyofanywa na TAWA wilayani humo.
“Kwa sasa wananchi wa wilaya ya Nkasi suala la kifuta jasho lipo asilimia 98, kuna wananchi 27 wanakwenda kulipwa hivi karibuni shilllingi Millioni Kumi na saba laki saba na elfu hamsini (17, 750,000/=) amesema Anorld Ngagashi
Anorld amesema mpaka sasa wananchi watatu kutoka Kata ya Kabwe (2) na Wampembe (1) wameshalipwa jumla ya shillingi Millioni tatu (3,000,000/=) malipo yaliyofanyika Desemba 20, 2024 na kusisitiza kuwa wananchi 24 waliosalia malipo yao yatakamilika muda wowote kuanzia sasa.
Aidha Afisa huyo amepongeza ushirikiano mkubwa wanaoupata kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA kupitia Pori la Akiba Lwafi katika kukabaliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu wilayani humo.
“Tunaishukuru Serikali hii ya Rais Samia pamoja na uongozi wa TAWA kwakweli tumeshirikiana 100%, kwahiyo Kati ya Mikoa yote mfano wa kuigwa ni Pori la Akiba Lwafi kwani wameonesha ushirikiano mkubwa kuhakikisha gurudumu hili la kupambana na wanyamapori wakali na waharibifu tunalisukuma wote Kwa pamoja” amesisitiza Ngagashi
Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja amesema licha ya matumizi ya teknolojia ikiwemo matumizi ya ndege nyuki TAWA imewekeza nguvu katika kuwapa elimu wananchi wanaoishi pembezoni mwa Hifadhi zilizo chini ya usimamizi wa Taasisi hiyo ili wapate uelewa wa namna ya kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu.
Aidha amesisitiza kuwa mbali ya changamoto ya miundombinu kwa vijiji hasa pale Askari wanapolazimika kuitumia kuvuka ili kuwafukuza wanyamapori waliovamia makazi ya watu, TAWA itahakikisha inafanya kila linalowezekana kuwafikia wananchi.
“Iwe jua iwe mvua TAWA tutapambana kuhakikisha tunaokoa maisha ya wananchi” amesisitiza Maganja
Wananchi wa Nkasi wamepongeza jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia TAWA katika kuhakikisha wanatoa elimu ya mbinu za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu hususani tembo Jambo ambalo wanakiri kuwa na msaada mkubwa katika kuokoa maisha ya wananchi hao.