Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thatib Kombo amepokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Canada nchini Mhe. Emily Burns katika Ofisi Ndogo za Wizara, jijini Dar es Salaam Desemba 23, 2024.
Akipokea nakala hizo Waziri Kombo amempongeza Mhe. Burns kwa uteuzi aliuopata na amemuahidi kumpa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake kwa kipindi atakachokuwa nchini kuiwakilisha nchi yake.
Aidha, Mhe. Kombo ameishukuru Canada kwa kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na Tanzania katika maeneo mbalimbali yakiwemo elimu, afya, ulinzi na usalama, utalii, biashara na uwekezaji.
Ameyataja maeneo mengine kuwa ni mabadiliko ya tabianchi, demokrasia, utawala bora na misaada ya kibinadamu; kwani yamesaidia kukuza diplomasia baina ya nchi hizo mbili.
Naye Balozi mteule wa Canada, Mhe. Burns ameishukuru Tanzania kukuza uhusiano wa kidiplomasia na Canada kwani umesaidia kuleta maendeleo kwa manufaa ya wananchi wa pande hizo mbili.
Mhe. Balozi Burns anachukua nafasi ya Balozi wa zamani wa Canada katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye amemaliza muda wake.