Na Sophia Kingimali.
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ametoa rai kwa wananchi wa mkoa huo kutembea na vitambulisho ili kurahisisha utambuzi wao katika matukio ya dharura huku akiwataka kusheherekea sikukuu ya krismasi na mwaka mpya kwa utulivu na amani pasipo kuvunja sheria wala kusababisha taharuki itakayopelekea kuharibu utulivu na amani iliyopo.
Wito huo ameutoa leo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam amesema jeshi la polisi limejipanga kuhakikisha usalama wa wananchi katika kipindi hiki cha sikukuu.
“Niwaombe wananchi wote wa mkoa huu kuhakikisha mnasheherekea sikukuu hizi mbili kwa amani na utulivu pasipo kuivunja amani ambayo ni tunu ya Taifa letu na amabae atataka kuivunja kwa makusudi basi jeshi la polisi limejipanga kuhakikisha wanalinda vizuri watu na mali zao lakini pia litawashughulikia watakaovunja amani ya taifa letu”,Amesema Chalamila.
Sambamba na hayo amewapongeza waandishi wa habari kwa mchango wao mkubwa katika kufikisha taarifa kwa jamii na kusaidia kujenga taifa kupitia ukosoaji wenye lengo la kujenga
Hata hivyo amewahimiza wanahabari kuwa waangalifu na taarifa wanazozitoa, hasa zile zinazohusu matukio ya utekaji.
“hivi karibuni la mtoto aliyeripotiwa kutekwa, lakini baadaye ilibainika kuwa alipatikana baada ya kuanguka kisimani na sio kutekwa kama ilivyokuwa imeandikwa kwa hiyo niwaombe tuwe makini na vyazo vinavyotoa taarifa hiyo”,amesema.
Aidha ameongeza kuwa hivi karibuni kulikuwa na tukio la mfanyabiashara Daisle Ulomi ambaye aliripotiwa kupotea na madai yakawa yanaonesha kama vile ametekwa, lakini uchunguzi wa polisi ulibaini baadae kwamba alipata ajali ya pikipiki.
Amesisisitiza umuhimu wa kushirikiana na vyombo vya usalama ili kudumisha amani hasa katika msimu huu wa sikukuu.
Akizungumzia mradi wa DMDP amesema tayari wakandarasi wameshakabidhiwa site na wanatarajia mwezi januari kuanza kazi kwa mujibu wa taratibu na sheria.
“Rais Dk Samia Suluhu Hassan anaendelea kutupatia fedha katika mkoa wetu wa Dar es salaam ili tuweze kutekeleza miradi mingi ya maendeleo na tutahikisha hatutamuangusha barabara zetu zilizoharibika zote zitarekebishwa na tayari wakandarasi wameshakabidhiwa maeno yao na tunatarajia januari waanze kazi”,Amesema chalamila.