* Ni ya Uzalishaji na Usafirishaji umeme
*Lengo ni kuhakikisha uwepo wa umeme wa uhakika
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Khatibu Kazungu ametembelea miradi mbalimbali ya uzalishaji na usafirishaji umeme inayoendelea kwa lengo la kufahamu utekelezaji wa miradi hiyo na maendeleo yake leo tarehe 21 Desemba, 2024 jijini Dar es Salaam.
Pamoja na kukagua miradi hiyo ya umeme inayoendelea, Dkt. Kazungu ametembelea vituo mbalimbali vya umeme kwa lengo la kuhakikisha kuwa vinafanya kazi ipasavyo na hivyo kuendelea kutoa uhakika wa uwepo wa umeme wa kutosha nchini.
Aidha, katika ziara hiyo Dkt. Kazungu amekagua mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia ya Ubungo I, II na III, na amekagua maendeleo ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Kimara – Ubungo – Mabibo hadi Ilala pamoja na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Mabibo.
Katika hatua nyingine, ametembelea kituo cha kupoza umeme cha Kinyerezi I, II na Kinyerezi I Extension pamoja na kukagua maendeleo ya ufungaji wa Transfoma ya ukubwa wa 175MVA katika kituo hicho.
Vilevile, ametembelea vituo vya kupoza umeme vya Gongo la Mboto na Mbagala na kukagua maendeleo ya ufungaji wa Transfoma zenye uwezo wa 120MVA kila moja katika vituo hivyo.