NA VICTOR MASANGU, BAGAMOYO
Katika kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita katika kuisaidia jamii Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu-ADEM imeamua kufanya ziara maalumu yenye lengo la kutembelea wafungwa katika gereza la Kigongoni lilipo Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani na kutoa misaada ya mahitaji ya msingi na vitu mbalimbali ambavyo vitawasaidia katika gereza hilo.
Akizunngumza Katika ziara hiyo mkurugenzi wa taaluma wa ADEM Bugendi Joseph amesema kwamba wamepata fursa ya kutembelea gereza hilo na kutoa mahitaji kama vile miswaki, dawa za meno, viwembe, sabuni, unga na mchele kwa kuzingatia mahitaji ya wafungwa.
Pia Bugendi amebainisha kwamba mbali na kutembelea gereza hilo pia watumishi pamoja na wanafunzi wa ADEM wametembelea kituo cha kulelea watoto wanaotoka katika mazingira magumu cha Amani Orphanage Center kilichopo katika Kata ya Zinga Wilayani Bagamoyo na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali ikiwemo vyakula, nguo, vifaa vya shule, na mahitaji mengine madogo madogo ya watoto wanaohudumiwa katika kituo hicho.
Aidha Mkurugenzi amesema sambamba na kukabidhi msaada huo uongozi wa Adem ukaamua kuchangia kiasi cha shilingi laki nane kwa ajili ya kuwasaidia katika kuboresha mazingira ya nyumba yao wanayoishi hasa miundombinu ya umeme.
Aidha, ziara hiyo pia imehusisha kutembelea Kaya zisizojiweza katika Kaya ya Kisutu, Bagamoyo ambazo zilibainishwa na Wenyeviti wa Mitaa katika Kata hiyo ambapo kaya zipatazo 13 zilisaidiwa mahitaji ya chakula na nguo.
Bugendi katika hatua nyingine amebainisha kwamba lengo la chuo hicho ni kuweka mikakati ya kuandaa wataalamu na viongozi mahiri ambao watakwenda kusaidia katika sekta ya elimu hapa nchini.
Naye Rais wa Serikali ya Wanafunzi-ASO Bw. Joshua Raphael mara baada ya kukamilika kwa ziara hiyo amesema, wao kama wanachuo wa ADEM kwa kushirikiana na Menejimenti ya ADEM wanaona fahari kubwa kushirikiana na jamii inayowazunguka hasa kwa kuisaidia jamii katika mshitaji mbali mbali.
Adem imekuwa mstari wa mbele katika kufanya Ziara kama hizo ambazo uwa zinafanyika kila mwaka ili kurudisha huduma kwa jamii na mskundi mbali mbali ikiratibiwa na Ofisi ya huduma saidizi za wanafunzi pamoja na Serikali ya Wanachuo wa ADEM-ASO.