Na Sabiha Khamis Maelezo 21.12.2024
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Dkt. Khalid Salum Mohamed ameitaka jamii kuwalinda na kuwatunza watoto ili kupata haki zao za msingi ikiwemo elimu na malezi bora.
Ameyasema hayo wakati akifungua Kiwanja cha kufurahishia watoto Paje Mkoa wa Kusini Unguja ikiwa ni shamrashamra za maadhimisho ya miaka 61 ya mapinduzi ya Zanzibar,amesema ni vyema kutunza na kuthamini juhudi za Serikali kwa kuwapatia watoto stahiki zao.
“Mtoto lazima ashirikishwe katika maamuzi, ahudumiwe katika makuzi yake yawe makuzi bora pia haki ya kupata elimu, haki ya kupata afya pamoja na haki ya kupata burdani na Serikali yetu imejitahidi katika hilo na haya ndio matunda ya Mapinduzi” alisema Dkt. Khalid.
Ameeleza kuwa kuwepo kwa kituo hicho kitaongeza pato la taifa pamoja na kufungua fursa za biashara kwa wananchi katika kujenga mahusiano mema na kuwapa watoto furaha, amani na utulivu.
Dkt. Khalid amesema madhumuni ya Mapnduzi ya January 1964 kuondosha ubaguzi, manyanyaso na mateso kwa wananchi wa Zanzibar na kuwaletea maendeleo na usawa na kuwafanya kuwa huru katika Nchi yao.
Akitoa taarifa ya kitaalamu Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Issa Mahfoudh Haji amesema kiwanja hicho kinauwezo wa kubeba nwatu 3000 kwa wakati mmoja na kitafanyakazi kwa skukuu na kila mwisho wa wiki.
Amesema kwa mwaka 2024 – 2025 Wiazra imetakiwa kujenga Viwanja vya kufurahishia watoto vitatu katika maeneo tofauti ikiwemo Paje katika Mkoa wa Kusini Unguja ambacho tayari kimezinduliwa vyengine ni Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja na Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo wenye lengo la kupunguza masafa na gharama kwa Watoto na Wananchi wa Mkoa wa Kusini kwa kufata huduma hiyo katika maeneo ya Mjini na kufungua fursa za ajira kwa wananchi ili kuisaidia Halmashauri kuingiza mapato na makusanyo ambayo ndio msingi wa kuendeleza na kuanzisha miradi mengine ya kimaendeleo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud amesema ujenzi huo utakamilika kwa muda mfupi kwa kukamilishwa kwa baadhi ya maeneo ikiwemo kuwekwa kwa uzio katika njia ya treni ili kuhakikisha usalama wa watoto pamoja na ujenzi wa bwawa la kuogelea ikiwa ni sehemu ya mafunzo ya kuogelea na kuongeza chachu ya michezo katika eneo hilo pamoja na kuongeza ofisi za utawala.
Amesema Mkoa huo upo katika hatua ya ujenzi wa bustani mbili za kupumzikia katika maeneo ya Jumbi na Hanyengwa mchana sambamba na kutarajia kuanzishwa kwa kituo chengine cha kufurahishia watoto Kizimkazi ambalo litatanua wigo kwa watoto kupata maeneo ya kupumzika na kucheza.
Zaidi ya Bilioni 1 zimetumika katika ujenzi wa mradi huo wa kiwanja chenye upana wa km 97 na urefu wa km 80 sawa na mita za mraba 7760.