Timu ya Simba SC imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 5- 2 dhidi ya wenyeji, Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara uliochezwa leo Disemba 21, 2024 katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba Mkoani Kagera.
Mabao ya Simba SC yamefungwa na beki Shomari Salum Kapombe dakika ya 13, viungo Muivory Coast Jean Charles Ahoua dakika ya 44, Mkongo Fabrice Luamba Ngoma dakika ya 53 na mshambuliaji Mganda Steve Dese Mukwala dakika ya 66 na 85.
Mabao ya Kagera Sugar yamefungwa na beki Datius Peter dakika ya 79 na kiungo Cleophas Anthony Mkandala dakika ya 90 + 3.
Kwa ushindi huo Simba SC imefikisha pointi 34 na kurejea kileleni mwa ligi kuu mbele ya Azam FC yenye pointi 33 za mechi 15 na mabingwa watetezi Yanga SC wenye pointi 30 za mechi 12.
Kwa upande wa Kagera Sugar baada ya kupoteza mchezo wamebaki na pointi 11 za mechi 15 kwenye ligi ya timu 16 ambayo mwisho wa msimu timu mbili zinashuka daraja.