Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. DENNIS L. LONDO (Mb.) amewataka watumishi wanaotoa huduma mipakani kufanya kazi kwa bidi, weledi na uadilifu. Mhe. Londo ametoa rai hiyo alipokuwa akiongea na watumishi wanaotoa huduma katika Kituo cha Utoaji Huduma kwa Pamoja cha Holili/Taveta, Wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea Vituo vya Kutoa Huduma kwa Pamoja Mipakani (OSBPs).
Akiwa katika mpaka huo, Mheshimiwa LONDO alijionea shughuli za biashara zinazofanyika mpakani hapo, miundombinu ya kituo hicho pamoja na kuongea na wafanyakazi wa Taasisi mbalimbali zinazotoa huduma kwenye mpaka huo.
Waziri LONDO amewasihi wafanyakazi hao kufanya kazi kwa maarifa, jitihada na kujiepusha na vitendo viovu ambavyo vinaweza kuchafua taswira ya nchi nje ya mipaka, pamoja na kukwaza ufanyaji biashara. Ametaja baadhi ya vitendo hivyo ni pamoja na rushwa na lugha zisizo na staha kwa wafanyabiashara na watumiaji wengine wa mipaka hiyo.
“Nyinyi watumishi wa mpaka huu wa Holili pamoja na mipaka yote nchini ni kioo cha nchi yetu katika kuhudumia wageni hivyo mnapaswa kufanya kazi zenu kwa weledi, bidii na maarifa makubwa ili kulinda taswira ya nchi yetu nje na ndani ya mipaka”. Alisisitiza Mhe. LONDO.
Aidha, Mheshimiwa Londo amewakumbusha watumishi hao wajibu wao katika kuwasaidia wafanyabiashara za mipakani kufikia malengo yao badala ya wao kuwa sehemu ya vikwazo na lugha zisizofaa wakati wa kuwahudumia. Vilevile, Mhe. LONDO amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa ushirikiano kwa taaisi zote za mipakani.
Kuhusu ushirikishwaji wa Halmashauri katika kuwezesha wafanya biashara wadogo kunufaika na fursa za Mtangamano wa Afrika Mashariki, Mhe. LONDO amezitaka Halmshauri kubuni mikakati ya jinsi kuwashirikisha wananchi wao kunufaika na uwepo wa mipaka hiyo katika Mikoa na Halmashajri zao. Mheshimiwa Londo amezitaka Halmashauri zilizo mipakani kujumuisha katika mipango na bajeti zake mikakati ya kuongeza tija na kuwawezesha wafanyabiaashara wa mipakani hususan vijana na akina mama kutumia kikamilifu fursa za Mtangamano wa Afrika Mashariki.
Akiwa katika mpaka huo wa Holili, Mhe. LONDO amekutana pia na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Rombo Mhe, RAYMONDI MANGWALA, wawakilishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mawakala wa Forodha wanaofanya shughuli zao katika mpaka wa Holili wa upande wa Tanzania na Kenya
Awali, akimkaribisha Mhe. Naibu Waziri, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Mhe. RAYMOND MANGWALA alimwelezea Mhe. LONDO kuwa Mpaka wa Holili upo salama na shughuli za biashara katika mpaka huo zinaendelea vizuri ambapo kumekuwa na ushirikaino mzuri miongoni mwa Taasisi zinazofanya kazi katika mpaka huo kiasi cha kupelekea mpaka huo kuwa miongoni mwa mipaka inayofanya vizuri katika kufikia malengo ya kiforodha.
Aidha, Mhe. MANGWALA hata hivyo alieleza changamoto kadhaa ikiwemo uwepo wa vipenyo vingi vinavyochochea biashara ya magendo na kubainisha kuwa pamoja na jitihada za Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya katika kukabiliana na vitendo hivyo, kuna umuhimu wa kutumia njia za kisasa za kitekenolojia katika kukubaliana na biashara za magendo katika Wilaya hiyo.