Kaimu Naibu Rais wa Ndaki ya Dar es Salaam akifungua mafunzo ya matumizi ya Ofisi Mtandao.
Mtoa mada katika Mafunzo Matumizi ya Ofisi Mtandao Bw. Alexander Benedicto.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya matumizi ya Ofisi Mtandao wakifatilia mafunzo kwa vitendo.
Picha ya pamoja ya washiriki wa mafunzo ya matumizi ya Ofisi mtandao na Kaimu Naibu Rais wa Ndaki ya Dar es Salaam Dkt. Coletha Komba (Katikati) baada ya kufunga mafunzo hayo
……..
Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam kimetoa mafunzo maalum kwa watunza Kumbukumbu na Maafisa Rasilimali Watu/Utawala kuhusu mfumo wa Ofisi Mtandao kwa watumishi wa umma wenye lengo la kuhakikisha wanazingatia Sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali ili kurahisisha utendaji kazi na kuepuka makosa ya uvujaji wa siri na taarifa kwa kutumia mifumo tumizi ya Serikali.
Akizungumza hayo Disemba 19, 2024 wakati wa kufunga mafunzo ya siku tano ya Matumizi ya Mfumo wa Ofisi mtandao na Uzingatia wa Sheria ya Matumizi ya Mifumo ya TEHAMA Serikalini kwenye taasisi za umma, Naibu Rasi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam, Dkt. Coretha Komba amesema mafunzo hayo yamelenga kuwaongezea uwezo washiriki wa mafunzo hayo katika masuala ya matumizi ya Ofisi Mtandao.
“Uadilifu katika kutekeleza majukumu ya kila siku ni muhimu sana ili kuweza kuchangia utendaji kazi bora katika Utumishi wa Umma hivyo ni lazima kuwa waadilifu na wawajibikaji”, amesema Dkt. Komba.
Mkufunzi wa Mifumo Tumizi ya TEHAMA Serikalini Bw. Alexander Benedicto ambaye ni Afisa TEHAMA Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu Mzumbe, amesema lengo la mafunzo ya matumizi ya Mfumo wa Ofisi Mtandao kwenye Taasisi za Umma ni kuwajengea uwezo watumiaji wa mfumo wa Ofisi Mtandao juu ya kutumia mfumo wenyewe na ulewa wa sheria ya matumizi sahihi ya mifumo tumizi ya TEHAMA ya Serikali.
Aidha Bw. Benedicto ameongeza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia Maafisa Rasilimali Watu wanaosimamia Masijala za Serikali kuwa na uelewa mpana wa mfumo na kuwa na uwezo wa kuona ripoti mbalimbali zilizomo kwenye mfumo ili kusaidia uendeshaji wa Ofisi zao lakini pia wataweza kuwasimamia vizuri watumishi wa masijala na wasimamizi wa mifumo ambao mara nyingine baadhi yao wanakuwa sio waaminifu katika utendaji kazi wao.
“Tumetoa mafunzo kwenu na kuhakikisha mnakuwa na uelewa mpana ili kusaidia taasisi zinapopata watumishi wapya au wanaohamia katika taasisi zenu ili muweze nanyi kuwapatia mafunzo, kwani tayari mfumo unakuwa na taarifa muhimu za taasisi hivyo kuwapa nafasi watu wengine ni kusema watakuwa wanaonyesha kazi za taasisi ambazo wanazo kwenye mfumo”.
Amesema kupitia mfumo huo Taasisi inaweza kutuma nyaraka kwa watumishi wake wote zikiwemo maamuzi ya baraza la wafanyakazi , vyama vya wafanyakazi ili waweze kuviona kwa pamoja bila kutuma kwenye email ambazo zimekuwa zikijaa.
Naye, Bw. Remidius Leonard Afisa Utumishi Mkuu Taasisi ya Ustawi wa Jamii kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, ameushukuru uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuandaa mafunzo hayo kwa ajili ya kuwaongezea uwezo katika kada zao wanazofanyia kazi.
“Washiriki wenzangu katika mafunzo haya kila kilichokuwa kinasisitizwa ni sehemu ya maadili, tumekuwa tunafanya makosa kwa kutozingatia maadili kwa hiyo tumetoka na kauli mmoja tukiahidi kwamba, maadili tutayazingatia ili tuweze kuboresha utendaji kazi wetu na kutoa matokeo chanya” Alisisitiza Bw. Leonard.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Chuo Kikuu Mzumbe na yameshirikisha Maafisa Rasilimali Watu, Maafisa TEHAMA, Watunza kumbukumbu na wasimamizi wa ofisi kutoka taasisi mbalimbali za Serikali hapa nchini.