Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesisitiza umuhimu wa sekta ya Maliasili na Utalii kama chanzo kikuu cha mapato ya Taifa na mhimili wa maendeleo ya kiuchumi nchini. Akizungumza jana (Ijumaa, Desemba 20, 2024) wakati wa uzinduzi wa Tuzo za Uhifadhi na Utalii uliofanyika katika Hoteli ya Mt. Meru, Arusha, Waziri Mkuu alibainisha kuwa serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuimarisha sekta hiyo.
“Tunatambua sekta ya maliasili na utalii kama chanzo kikubwa cha mapato ya taifa, ikichangia asilimia 21.5 ya pato ghafi la Taifa, ambapo asilimia 17.2 ni utalii na asilimia 4.3 ni misitu na nyuki,” alisema Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu aliongeza kuwa sekta hiyo pia inachangia asilimia 30.9 ya mapato ya fedha za kigeni, huku asilimia 25 ikitokana na utalii na asilimia 5.9 kutoka kwenye misitu na nyuki.
Katika hotuba yake, Mheshimiwa Majaliwa aliipongeza serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kuinua sekta ya utalii, ambazo zimewezesha ongezeko kubwa la idadi ya watalii wa kimataifa. Takwimu zinaonyesha ongezeko la asilimia 96 ya watalii kutoka 922,692 mwaka 2021 hadi 1,808,205 mwaka 2023, huku mapato yatokanayo na utalii wa kimataifa yakiongezeka kwa asilimia 68.2, kutoka dola bilioni 2.0 mwaka 2021 hadi bilioni 3.4 mwaka 2023.
“Rais Dkt. Samia amefanikisha mageuzi makubwa katika sekta ya utalii, huku filamu ya The Royal Tour ikiwa moja ya nyenzo zilizochochea mafanikio haya,” alisema Majaliwa.
Alitoa wito kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha kuwa vigezo vya utoaji wa tuzo hizo vinawekwa wazi na kuzingatia ubora katika maeneo kama uhifadhi wa mazingira, usimamizi wa hifadhi za wanyamapori, na huduma za utalii.
Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana, alisisitiza kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha sekta ya maliasili na utalii inaendelea kukuwa kwa kasi, akimpongeza Rais Samia kwa uongozi wake thabiti na maono makubwa katika sekta hiyo.
Tuzo za Uhifadhi na Utalii zimeanzishwa kwa lengo la kuongeza ushindani miongoni mwa wadau wa sekta hiyo, hatua ambayo inatarajiwa kuimarisha ubunifu na kuongeza ubora katika utoaji wa huduma.