Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (Mb), akiweka jiwe la Msingi la Ujenzi wa Daraja la Sukuma
lenye urefu wa Mita 100 pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 2.3 leo tarehe
20 Desemba 2024. Kushoto ni Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya (Mb) na
viongozi wengine wa Chama na Serikali wakishuhudia zoezi hilo.
Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya (kulia) akitoa salamu kwa wananchi mara
baada ya kuwekwa jiwe la Msingi la Ujenzi wa Daraja la Sukuma lenye urefu wa Mita 100
pamoja na barabara unganishi yenye urefu wa kilometa 2.3. Kushoto ni Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mohamed Besta akitoa
taarifa ya Ujenzi wa Daraja la Sukuma lenye urefu wa Mita 100 pamoja na barabara unganishi
yenye urefu wa kilometa 2.3 kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (kushoto). Wengine ni Naibu
Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya (wa tatu kushoto) na Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Ujenzi Dkt. Charles Msonde (wa pili kulia).
Muonekano wa Daraja la Sukuma lenye urefu wa Mita 100 pamoja na barabara unganishi zenye
urefu wa kilometa 2.3, ambalo ujenzi wake unaendelea.
……..
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Daraja la Sukuma lenye
urefu wa Mita 70 na barabara unganishi Kilometa 2.3 na kusisitiza kuwa Serikali ipo imara na
inaendelea kuwahudumia watanzania na kuhakikisha huduma muhimu za kijamii zinawafikia
watanzania wote.
Akizungumza Desemba 21, 2024 katika kjjiji cha Ngh’aya, wilayani Magu mkoani Mwanza,
wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huo, Majaliwa amesema kuwa ujenzi unaenda
vizuri na kuwahakikishia wananchi kuwa mradi huo utakuwa mkombozi kwa watu wa Magu na
wilaya za jirani.
“Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika kwa
kupelekewa huduma muhimu katika eneo lake ikiwemo barabara, madaraja, zahanati na shule”,
amesema Majaliwa.
Aidha, Majaliwa ameeleza kuwa Utekelezaji wa miradi hiyo unaonesha namna Serikali
inavyofanya kazi kwa kuleta maendeleo nchini.
Katika hatua nyingine Majaliwa amekagua ujenzi wa daraja la Simiyu lenye urefu wa mita 175
na barabara unganishi yenye urefu wa Kilometa 3 ambapo amesema kuwa Serikali imeona
umuhimu wa kujenga daraja hilo ambalo lilijengwa tangu enzi ya mkoloni na kuamua kulijenga
upya na kuwa la kisasa.
Aidha, amewataka Wakala wa Barabara (TANROADS) kuhakikisha wanasimamia miradi hiyo
ili ikamilike kwa wakati.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema kuwa
Ujenzi wa daraja hilo utasaidia kupunguza ajali kwa kiasi kikubwa kutokana na kwamba daraja
la zamani lilikuwa na njia moja ila la sasa litakuwa na njia mbili.
Ameongeza kuwa Ujenzi wa madaraja hayo ni moja ya utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya
kuboresha sekta ya miundombinu nchini ambapo daraja la Sukuma limefika asimia 24 na Simiyu
limefika asilimia 35 ambayo yote yanagharamiwa na Serikali kwa asilimia 100.
Amefafanua kuwa kukamilika kwa madaraja hayo kutarahisisha usafiri na usafirishaji wa watu
na bidhaa pamoja na kukuza na kuchochea uzalishaji katika sekta za kilimo, madini na viwanda.
Waziri Mkuu amefanya ziara ya ukaguzi na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali
mkoani Mwanza ikiwemo ujenzi wa daraja la Sukuma na Simiyu ambayo yanagharamiwa na
Serikali kwa asilimia 100.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Ujenzi