Na Sophia Kingimali.
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Vijana ,Ajira na Watu wenye ulemavu),Ridhiwani Kikwete amewataka vijana kufanya bunifu ambazo zitakuwa na tija kwa Taifa lakini pia ziatakazowafanya kupata kipato lakini pia kujulikana kimataifa na serikali imejipanga kuwawekea sera nzuri lakini pia kusapoti bunifu zao kwa kuwapatia mitaji.
Aidha amesema hajisikii vizuri vijana kuona vijana wanakosa mitaji katika kufanya bunifu zao licha ya serikali kufanya harakati ya kuwekeza fedha nyingi kwenye kukuza ubunifu.
Hayo ameyasema leo Disemba 20,2024 jijini Dar es Salaam wakati akifunga maadhimisho ya wiki ya Startup, amesema unapozungumzia suala la ubunifu halimlengi kijana pekee ake bali anaweza kuwa mtu mzima katika kufanya ubunifu huo.
Amesema shida inaweza kuwa kwao ambao wapo katika utekelezaji kushindwa kuwapa taarifa vijana juu ya fursa zilizopo ndani ya Serikali.
Amesema tayari amewaelekeza watumishi wenzake ofisini jambo hilo lazima walifanye katika kuhakikisha vijana wanawezeshwa kiuchumi.
“Mfano kuna mfuko wa vijana ambao unalenga kusaidia bunifu zinazofanywa kama hizi,Vijana wanaanzisha bunifu zao lakini wanashindwa kuzikuza kwa sababu hawana mitaji sasa ukiangalia unachokiona hapa,unakuta vijana wanabuni kitu chao huku anatafuta hela kwaajili ya kufanya production ya vifaa anakosa hela,”amesema.
Ameongeza kuwa sio kweli kwamba serikali haiwezi kumsaidia kijana huyo kwani ni kazi ya Serikali kufungua milango na kutengeneza mazingira mazuri ya hata watu binafsi kuwasaidia watu hao.
Amesema ni vema kuendelea kuwatia moyo watu binafsi kujua serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imefanya jambo moja kubwa ambalo imelifanya ni kutengeneza mazingira ya wawekezaji na wawezeshaji kuja na kushirikiana na watanzania katika kuhakikisha mambo yanaenda vizuri juu ya ubunifu.
Sambamba na hayo amesema wizara watahakikisha Wanatengeneza mazingira mazuri ya Startups kukua,kwani Startups ni sehemu ya biashara zinazolenga kukua kwa haraka zaidi kwa kutumia bunifu mpya na za kiteknolojia kwa kuleta suluhisho jipya,na kwa haraka zaidi.
Amesema agosti mwaka huu wamezindua sera ya vijana ambapo sera hii katika moja ya jambo kubwa inazungumza ni kuwezesha bunifu mbalimbali.
Amesema mtu hawezi anzisha bunifu kama haujui ndani ya bunifu hizo zinafanyika kitu gani hivyo ni jambo ambalo katika awamu ya pili inayokuja ni programu ya usambazaji wa kutoa elimu ya vijana kuelewa kwamba sera yenyewe inazungumza vitu gani au wadau muhimu kuelewa kwa undani juu ya sera hiyo na kuja kuchangia baadae.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Startups Association Zahoro Muhaji amesema kuwa Tamasha hilo limekua na mafanikio makubwa na kwamba Startups imekua ikichangia pato la taifa na ajira ambapo kwa miaka 4 tangu kuwepo kwa Startups nchini imeweza kuchangia uwekezaji wa dola milioni 3 na ajira za kazi laki moja mpaka sasa.