Na Mwandishi wetu, Hanang’
MBUNGE wa Jimbo la Hanang’ Mkoani Manyara, mhandisi Samwel Hhayuma amesema wananchi wa eneo hilo wanashukuru mno Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwasaidia kipindi cha maporomoko ya tope yaliyotokea Desemba 3 mwaka 2023.
Mhandisi Hhayuma akizungumza kwenye uzinduzi na kukabidhi nyumba 109 za waathirika katika kitongoji cha Waret, Kijiji cha Gidagamowd, mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema wananchi wa Hanang’ wanamshukuru mno Rais Dkt Samia.
“Tunamshukuru Rais Dkt Samia alikuwa nje ya nchi na kuahirisha ziara yake nje ya nchi japokuwa angeweza kutuma mwakilishi ila alifika na kabla aliagiza Mawaziri 17 wahamie Hanang’ ili kupambana na maafa hayo,” alisema Hhayuma.
Amesema ili kuonyesha mapenzi mema waliyonayo wananchi wa Hanang’ wanampa Rais Dkt Samia zawadi ya ndoo ya lita 20 ya asali na Waziri Mkuu Majaliwa wamempatia pia lita 20 ya asali.
Hata hivyo, amesema Hanang’ inazidi kupiga hatua ya maendeleo kwenye sekta ya elimu, afya, miundombinu ya barabara na maeneo yote yanakwenda sawa.
Ametoa ombi juu ya mashamba makubwa ambayo hayatumiwi na wawekezaji wapatiwe wakulima kipindi hiki cha kilimo na pia suala la ugawaji mbegu kwenye ruzuku lisiwe gumu ili wakulima wapatiwe.
Mhandisi Hhayuma amesema wanahitaji kituo cha kituo cha kupooza nishati ya umeme ili kujengwe viwanda vya kusindika chumvi na saruji.
Amesema wananchi wa Hanang’ hawana kitu cha kumlipa Rais Dkt Samia ila wanaahidi kuwa mwaka 2025 wapo na Rais Samia kwenye uchaguzi mkuu wa nafasi hiyo.
Katika makabidhiano hayo ya nyumba 109 na hati za viwanja, pia walipatiwa mitungi ya gesi 109, ambapo watu 745 wataishi kwenye nyumba hizo.
Nyumba hizo zimejengwa baada ya Rais Samia kutoa ahadi kuwa Serikali itajenga nyumba baada ya kutokea maafa ya tope Desemba 3 mwaka 2023.