Na Dotto Mwaibale, Dar es Salaam
KAMPUNI ya Ndege Tanzania (ATCL) imeinua uchumi na kuiunganisha
Tanzania na mataifa mengine kufuatia kufanya vizuri katika biashara
ya usafiri wa anga kwa kusafirisha abiria na mizigo ndani na nje ya nchi.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na
Msemaji wa Serikali, Geryson Msigwa wakati akitoa taarifa kuhusu masuala
mbalimbali yaliyotekelezwa na Serikali katika mkutano na waandishi wa habari
uliofanyika Desemba 19, 2024 jijini Dar es Salaam.
“ Uwepo wa ndege za kisasa 16 (Abiria 15 na mizigo1)
zilizonunuliwa na Serikali zimekua kichocheo katika kuboresha na kuimarisha
sekta ya usafiri wa anga Tanzania,” alisema Msigwa.
Msigwa alisema mpaka sasa Kampuni ya Ndege Tanzania ina ndege
Boeing 767 – 300F (Mizigo) 1, Boeing 737 – 9 Max 2, Boeing 787 – 8 (Dreamliner)
3, Airbus 220 – 300 4, DE Havilland Q400 5, DE Havilland Q300 1 na kueleza kuwa
Ndege hizo zinafanya safari katika vituo 27 ambapo 15 ni vituo vya ndani
ya nchi (Mikoa) pia vituo vya nje ya nchi ikiwemo (Africa (9), Nje ya
Afrika (3) – Dubai, Mumbai na Guangzhou)
Katibu huyo Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo alitaja mafanikio ya uendeshaji wa ndege hizo
kuwa katika kipindi cha kutoka Januari mpaka Desemba 17, 2024, ATCL imefanikiwa
kusafirisha abiria 1,109,803, mizigo tani 10,181 na kufanya safari za ndani na
nje ya nchi 16,522.
Alisema Usalama na Utendaji ATCL ina vibali vya usalama wa
kufanya safari katika vituo takribani 12 vya nje ya nchi.
Aliongeza kusema kwamba ATCL imeendelea kushirikiana na
wataalamu wa ndani na nje ya nchi ikiwemo Kampuni za kuunda ndege (Boeing na
Airbus) ambao wamekuwa wakisaidia kutoa mafunzo na kufanya mapitio ya uendeshaji
wa shughuli zake kwa kuzingatia taratibu za usalama.
“ATCL imeendelea kufanya mashirikiano na mashirika makubwa ya
ndege ikiwemo Emirate Airlines, Ethiopian Airline, Air India, Qatar, Airways,
APG Airline, Hahn Air, Oman Air, Rwanda Air, Egypt Air, Proflight Zambia, LAM –
Mozambique Airlines, na Fly Dubai, Ufufuaji wa ATCL umesaidia kukuza sekta
mbalimbali ikiwemo utalii kwakutangaza vivutio vyetu na kuwawezesha watalii
kufikia vivutio hivyo,” alisema Msigwa.