Na Sophia Kingimali.
RAIS Dkt Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza maadhimisho ya miaka 25 ya Chama cha Majaji wanawake Tanzania (TAWJA) yanayotarijiwa kufanyika Arusha huku yakiongozwa na kauli mbiu isemayo ‘Kusheherekea utofauti na mshikamano katika usawa wa jinsia’
Pia,Maadhimisho hayo yatafanyika kwa siku tano kuanzia Januari 19-23, 2025 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa jijini Arusha na yatatanguliwa na Marothoni ambapo Spika wa bunge Dk Tulia Ackson anatarajiwa kuongozea mbio hizo.
Akizungumzia tukio hilo leo Disemba 19,2024 Mwenyekiti wa TAWJA Jaji wa Rufani Barke Sahel amesema siku hiyo masuala mbalimbali yatajadiliwa ikiwamo masuala ya haki na usawa wa kijinsia.
Akizungumzia kuhusu kesi ambazo zimekuwa zikijirudia kila siku Jaji Sehel amesema ni ongezeko la kesi za ubakaji na ulawiti ambazo miaka ya hivi karibuni zimekuwa zikiongezeka.
“Kwenye maadhimisho haya tutaeleza changamoto mabalimbali ikiwamo hii ya ongezeko la kesi za ubakaji na ulawiti na nini kifanyike ili kutokomeza hali hiyo,” amesema.
Amesema, hivi sasa matukio ya ubakaji na ulawiti yameongezeka kwenye mikoa karibu yote nchini.
“Miaka ya nyuma kesi za namna hii zilisikika kwenye baadhi ya mikoa, lakini miaka ya huvi karibu karibu mikoa yote inamatukio haya tena kwa kiwango cha juu,”.
“TAWJA tunafanya jitihada kuhakikisha changamoto hizi zinatatuliwa katika nyanja mbalimbali ikiwamo kutoa elimu kwenye masuala ya usawa wa kijinsia,” amesema.
Akizungumzia miaka 25 ya Chama hicho, Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo Taifa, Sophia Wambura amesema katika kipindi hicho TAWJA imefanikiwa kukuza hali ya usawa kwenye ngazi ya utendaji wa Mahakama.
“Vilevile tumehamasisha usawa kwenye jamii katika kuijengea uwezo kutambua haki zao katika mirathi, talaka na haki za usawa na masuala mengine ya kijamii,” amesema.
Hata hivyo Jaji wa Mahakama Kuu kanda ya Arusha na mwenyekiti wa kamati mwenyeji ya maandalizi ya maadhimisho hayo, Aisha Bade amesema bado kuna changamoto za dhamana.
Amesema pamoja na kwamba dhamana zinakua wazi lakini wahusika wanashidwa kutimiza masharti ya dhamana kwa kukosa baadhi ya mahitaji kama mdhamini na vitambulisho, jambo ambalo katika maadhimisho hayo pia watatoa elimu hiyo.
Maadhimisho hayo pia yatashirikisha wadau wengine ikiwamo majaji na mahakimu wanawake kutoka Bara na Zanzibar sambamba na washirika wa kimataifa kama UN Woman, UNDP na UNICEF.