Na Prisca Libaga Arusha
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mount Meru, imepokea dawa na vifaa tiba pamoja bidhaa zingine vyenye thamani ya shilingi million 15 kutoka kwa Watumishi wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa Tanzania TAKUKURU kwa lengo la kusaidia kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa kabla ya Wakati.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mt. Meru, Mkurungezi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania TAKUKURU Bw Chrispin Chalamila amesema kuwa yeye na Watumishi wenzake wametoa vifaa tiba, dawa pamoja na mahitaji Mengine muhimu kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati ili kusaidia kupunguza Changamoto na gharama ya kuwatunza watoto hao.
“Sisi Watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania tumeamua kujichangishana fedha na kufikisha jumla ya shilingi Milioni 15 ambazo tumezitumia kununua mashine yakuwapatia watoto joto, dawa, vifaa tiba pamoja mahitaji mengine ya muhimu ili kurahisisha zoezi la kutoa huduma ya afya na kupunguza gharama ya kuwahudumia watoto wanaozaliwa kabla ya Wakati” amesema Chalamila.
Pia Chalamila amewataka Watanzania kuwa na moyo wa uzalendo kwa kujitokeza kuzisaidia taasisi za umma pamoja na wale ambao hawana uwezo wa kugharamia matibabu kwani kutaipunguzia serikali gharama ikizingatiwa kwamba serikali inahudumia taasisi nyingi na kwa kufanya hivyo kutarahisisha zoezi la utoaji wa huduma za afya.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa Mount Meru, Dkt. Alex Ernest amewashukuru Watumishi wa TAKUKURU kwa Michango yao iliyofanikisha na ununuzi kifaa cha kuwapatia watoto joto, dawa pamoja mahitaji muhimu kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati kwani si tu inaongeza ufanisi na uhakika wa utoaji wa huduma lakini pia inaleta ahueni kwa wazazi ambao hawawezi kumudu gharana za mahitaji muhimu kwa watoto ikiwa ni pamoja na Virutubisho lishe bidhaa zingine muhimu.
Dkt. Alex amesisitiza kuwa michango hiyo itatunzwa na kutumika ipasavyo ili viweze kudumu na kusaidia Watanzania wengi.
Pamoja na hayo Watumishi TAKUKURU wametembelea jengo la huduma za dharura kwa viongozi, watalii pamoja na watu Maalumu ambapo wamevutiwa na ubunifu na uwekezaji wa vifaa vya teknolojia ya kisasa vya utoaji wa huduma za Afya
Shughuli hiyo imehitimishwa kwa upandaji wa miti ambayo itaboresha mazingiara ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mount Meru, ambapo Mkurungezi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania TAKUKURU Chrispin Chalamila ameongoza zoezi hilo.