Na Prisca Libaga Maelezo Arusha
BENKI Kuu ya Tanzania (BOT) inatarajia January mwakani kuzindua mfumo mpya wa kielektroniki unaolenga kuboresha huduma kwa wateja na kushughulikia changamoto zinazotokana na huduma za kibenki hapa nchini ambapo mfumo huu unatarajiwa kuwa suluhisho la haraka na lenye ufanisi katika kushughulikia malalamiko ya wateja wa sekta ya fedha.
Akifungua warsha ya siku mbili ya kuwajengea uelewa taasisi za benki mkoani Arusha ,Meneja wa Idara ya Uchumi Benki Kuu ,Arusha ,Aristedes Mrema, amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha uaminifu katika sekta ya fedha ambapo malalamiko ya wateja yatashughulikiwa kwa njia rahisi na ya haraka.
Amesema Mfumo huu unatarajiwa kupunguza usumbufu wa kufuatilia malalamiko kwa njia za kawaida, ambapo wateja mara nyingi walilazimika kutumia muda mwingi kufika benki kuu.
Mfumo huu mpya unahamasisha matumizi ya teknolojia katika sekta ya kifedha, ikiwa ni moja ya juhudi za serikali kukuza uchumi wa kidijitali.
Mrema, amesema kuwa Benki Kuu ya Tanzania imekabidhiwa jukumu la kuwalinda watumiaji wa huduma za kifedha, pamoja na majukumu mengine kama vile kuimarisha huduma jumuishi, usimamizi wa taasisi za fedha na uthabiti wa fedha.
Amesema uwepo wa mfumo huo ni nyongeza kwa juhudi zinazoendelea ambazo Benki inafanya kuhakikisha uaminifu katika sekta ya fedha kupitia mwongozo madhubuti wa kushughulikia malalamiko, mwenendo wa soko, na pia juhudi za kuongeza uelewa wa kifedha kwa watumiaji wetu
Mrema,amesema kwa kutumia teknolojia, Benki imetengeneza Mfumo wa Utatuzi wa Malalamiko ya wateja wa huduma za Kifedha ili kuboresha mchakato wa kushughulikia malalamiko kwa njia bora, ya haki, na inayoweza kufikiwa kwa urahisi, hivyo kukuza uaminifu, ushirikishwaji wa kifedha, na uthabiti wa fedha.
Amesema kuwa hatua hiyo ni muhimu sio tu katika kurahisisha uwasilishaji wa malalamiko na watumiaji bali pia kuimarisha uzingatiaji wa uwasilishaji wa malalamiko kutoka kwa taasisi zenu kama inavyotakiwa na Kanuni za Benki Kuu ya Tanzania za kumlinda Mtumiaji wa Huduma za Kifedha, 2019.
Mrema,amesema kuwa ushiriki wa dhati na umiliki wa mfumo huo katika warsha hiyo ni wa umuhimu mkubwa, kwa kuwa mfumo huo unazingatia mahitaji ya watumiaji wa huduma za kifedha ambao unahitaji watumiaji wa huduma hizo na Taasisi za Huduma za Kifedha (FSPs) kuuuelewa na kuutumia kwa ufanisi.
Amesema baada ya warsha watakuwa na uwezo wa kutumia mfumo huo katika shughuli zao za kila siku wakati wanapotekeleza jukumu la kulinda watumiaji wa huduma za kifedha.
Amesema ana imani kuwa mfumo huu utakuwa kama alama ya matumaini kwa watumiaji, jukwaa la mazungumzo ya kujenga, na kichocheo cha maboresho zaidi katika sekta ya fedha.
Mrema, akawataka washirikiane kuhakikisha mafanikio ya mfumo huo kama hatua ya kuimarisha uhusiano kati ya watoa huduma za kifedha na wateja wao, na kama ishara ya kujitolea kwao kuendeleza mazingira endelevu na yanayoaminika ya kifedha nchini.