Na Silivia Amandius.Kagera.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, ametoa wito kwa wananchi wa Kagera waliopo ndani na nje ya mkoa huo kuendelea kuwaunga mkono wawekezaji ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa unaojivunia fursa nyingi za kiuchumi.
Akizungumza katika jukwaa la uwekezaji mkoani Kagera, lililokuwa sehemu ya tamasha la IJUKA OMUKA, Biteko amesisitiza umuhimu wa kuondoa vikwazo vinavyokatisha tamaa wawekezaji. Alisema fursa zilizopo mkoani humo, hasa kutokana na ukaribu wake na nchi za Afrika Mashariki, ni za kipekee.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatuma Mwasa, amewahimiza wawekezaji kutumia fursa za kijiografia za mkoa huo, akibainisha kuwa uwekezaji katika sekta kama uvuvi, viwanda, na kilimo unaweza kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi.
Aidha, miradi ya kimkakati kama ujenzi wa stendi ya kisasa, soko jipya, na kingo za Mto Kanoni imeelezwa kuwa tayari iko kwenye hatua za utekelezaji, huku baadhi ya sekta zikionyesha mafanikio, kama vile ufugaji wa vizimba vya samaki na utafiti wa njia bora za uvunaji wa senene.
Tamasha la IJUKA OMUKA limebeba ujumbe wa kuwakumbusha wenyeji wa Kagera umuhimu wa kurudi nyumbani na kushiriki katika maendeleo ya mkoa kwa kuwekeza rasilimali zao ili kuchochea uchumi wa mkoa huo.