Wenyeviti wa mitaa mbalimbali katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza wakiwa kwenye mafunzo ya kujengewa uwezo yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo katika Halmashauri hiyo
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi akizunngumza kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo wenyeviti wa mitaa, kushoto ni Mkurugenzi wa Tafti Shauri elekezi na mafunzo ya muda mfupi Bahati Mfungo
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi, amewataka wenyeviti wa mitaa kujiepusha na utendaji kazi usiozingatia sheria,kanuni na taratibu hatua itakayosaidia kuepuka migogoro isiyo ya lazima.
Makilagi ametoa Rai hiyo Leo Ijumatano Disemba 18, 2024 wakati akifungua mafunzo ya siku moja yaliyolenga kuwajengea uwezo wenyeviti wa mitaa 175 iliyoko kwenye Kata 18 katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Alisema wenyeviti wa mitaa wanawaongoza wananchi katika shuguli mbalimbali za kijamii pamoja na kuwaletea maendeleo hivyo hawapaswi kuwa chanzo cha migogoro.
“Uongozi unahitaji busara na kuridhika na hali ya maisha uliyonayo kazi ya kuuza viwanja siyo kazi ya mwenyekiti wa mtaa,ndio maana huwa mnasababisha migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikileta kero kwa wananchi mnaowahudumia”, Alisema Makilagi
Aidha, aliongeza kuwa miongoni mwa kazi za wenyeviti wa mitaa ni kuibua miradi mbalimbali katika maeneo yao ambayo italeta tija kwa wananchi.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Bi. Witness Malero aliwaomba wenyeviti kuwa waadilifu wanapowahudumia wananchi sanjari na kuzingatia maadili ya kazi.
Naye Mkurugenzi wa Tafiti,Shauri elekezi na Mafunzo ya muda mfupi kutoka Chuo Cha Serikali za Mitaa Dodoma, Bahati Mfungo alisema mafunzo hayo ni muhimu sana kwa wenyeviti wa mitaa kwani yanawasaidia kuwakumbusha majukumu yao ya kazi na kujifunza vitu vipya ambavyo vinakuwa vimebadilika ikiwemo sera na miongozo.
Machoke Mwita mwenyekiti wa mtaa wa Mlimani na Zainabu Alphani wa mtaa wa Karuta ni miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo, walisema mafunzo hayo yatawasaidia kufanya kazi zao vizuri huku wakiahidi kushirikiana vizuri na wananchi.