Na Mwamvua Mwinyi
Disemba 18,2024
Wananchi mbalimbali wametembelea banda la Benki ya CRDB katika Maonesho ya Nne ya Wiki ya Biashara na Uwekezaji yanayoendelea mkoani Pwani, ambapo wamepata fursa ya kupata maelezo kuhusu huduma ya uwekezaji kupitia hati fungani ya SAMIA MIUNDOMBINU BOND.
Hati fungani hiyo, inayolenga kukusanya fedha kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za serikali kuboresha miundombinu ya barabara kwa kushirikiana na TARURA, inatoa nafasi ya uwekezaji wa miaka mitano wenye faida ya asilimia 12 kwa mwaka. Malipo ya faida yanalipwa kila baada ya miezi mitatu moja kwa moja kwenye akaunti za wateja.
Uwekezaji kupitia hati fungani hiyo unaruhusu kuanzia kiwango cha chini cha shilingi 500,000 bila ukomo, hivyo kuwa nafasi nzuri kwa wananchi kuwekeza na kupata faida huku wakichangia maendeleo ya taifa.
Maonesho hayo yamefunguliwa rasmi Disemba 17 na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo (Mb), na yanatoa jukwaa muhimu kwa wananchi na wawekezaji kuelewa fursa mbalimbali za uwekezaji na biashara.
Banda la CRDB limevutia idadi kubwa ya wananchi wanaopata elimu ya kifedha na kuelewa jinsi ya kushiriki katika maendeleo ya miundombinu kupitia hati fungani hii ya kipekee.