Na Sophia Kingimali.
Waziri wa nchi Ofisi ya waziri mkuu (kazi, vijana, Ajira na Wenye Ulemavu)Ridhiwani Kikwete ametoa rai kwa vijana nchini kushiriki kikamilifu katika uhakiki wa Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ili kuiendea Tanzania wanayoitaka.
Hayo ameyasema leo Disemba 18,2024 jijijni Dar es salaam wakati akifungua mkutano wa Mtandao wa vijana kuhakiki Rasimu ya Dira ya Maendeleo 2050 ambao umewajutanisha vijana kutoka sehemu mbalimbali nchini.
Amesema vijana wanapaswa kuyabainisha mambo ambayo Dira hiyo haijazungumzia lakini pia kushauri maboresho yanayopaswa kufanyika ili kuhakikisha masuala ya vijana yanawasilishwa ipasavyo.
“Lazima vijana mjue kama kuna maeneo ambayo hayakusemwa vizuri ni nafasi yenu kuyasema kwa uwazi lakini pia kwenye uhakiki yapo maeneo ambayo tunadhani hayakuelezwa vizuri sasa hii ni nafasi yetu kama vijana kuyaeleza vizuri”,Amesema Ridhiwani.
Sambamba na hayo amewapongeza waandaji wa Rasimu hiyo huku akiwataka kuhakikisha wanakutana na makundi na wadau wote nchini katika zoezi hilo la uhakiki.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa mipango kitaifa kutoka Tume ya Mipango Anjela Shayo amesema uwepo wa vijana katika uhakiki wa Rasimu hiyo ni kuhakikisha yale mambo makuu yanayohusu vijana kama yamezingatiwa.
Amesema timu ya uandishi wa dira ya 2050 imejipanga kupokea maoni kutoka kwenye makundi mbalimbali lengo kuhakikisha wanafikia kila kundi.
“Sisi tunaamini Dira hii ni ya vijana kwani asilimia 80 ya maoni tuliyoyapokea yametoka kwa vijana kwani wao ndio wenye mambo mengi ikiwemo uchumi jumishi,Ajira,uwezeshaji na mazingira wezeshi ya biashara haya yote yanamgusa kijana na ndio maana tunasema dira hii ni ya vijana”,Amesema.
Aidha ameongeza kuwa vijana waliokutana nao ni kutoka sehemu mbalimbali nchini hivyo lengo la kupata maoni kutoka kwa vijna litatimia na wanatarajia kupata maoni mengi yenye kujenga.
Naye,kijana kutoka shirikisho la watu wenye Ulemavu idara ya vijana nchini Abdallah Kameta amesema Dira ndio maendeleo hivyo anatarajia kupitia dira hiyo ya 2050 itaweza kutatua changamoto nyingi wanazokutana nazo vijana.
“Sisi tunaamini Dira ndio Maendeleo na hasa kwa vijana maana Taifa la kweli linajengwa na vijana hivyo naamini kupitia vizuri Rasimu hii itatusaidia kutoa maoni yetu ili kuelekea dira ya maendeleo 2050”,Amesema Kameta.