Na Mwandishi wetu, Babati
MTANDAO wa vikundi vya wakulima na wafugaji Mkoa wa Manyara (MVIWAMA) umefanya mkutano wao wa 17 uliofanyika mjini Babati.
MVIWAMA ni jumuiya ya wanachama inayolenga kutetea maslahi ya wakulima, wazalishaji wa mazao ya mimea, mifugo na samaki wadogo.
Mkutano huo wa 17 wa MVIWAMA umeshirikisha wanachama wawakilishi 128 kutoka wilaya za Babati, Simanjiro, Kiteto Hanang’ na Mbulu
Mratibu wa MVIWAMA, Valentine Ngorisa, akizungumza mjini Babati amesema kauli mbiu yao ni nguvu ipo tuwapo wengi na uwezo upo pamoja.
Ngorisa amepongeza hatua za serikali za kupunguza tozo mbalimbali katika kilimo, kuboresha miundombinu, kuimarisha upatikanaji wa nishati mijini na vijijini na kuanzisha mfumo wa elimu bure.
“Kwa uhakika mfumo huo wa elimu bure utawawezesha watoto wa wakulima na watu wengine masikini kupata elimu ya msingi na sekondari na ni matumaini yetu kwamba hatimaye serikali itaweka mfumo kama huo katika ngazi ya chuo kikuu,” amesema Ngorisa.
Ametumia fursa hiyo kuipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufuta umiliki wa ardhi ambayo imekuwa ikihodhiwa na wachache wakati wakulima walio wengi hawana ardhi ya kufanyia shughuli za kilimo na ufugaji.
“Tunamshukuru sana na kumuomba hatua hiyo ya Rais Samia iendelee kwa sababu bado kuna maeneo mengi ambayo yanahodhiwa na wachache huku wananchi wengi hawana ardhi kwa ajili ya uzalishaji na wengine wakikodishwa ardhi yao wenyewe na wanaojiita wawekezaji.
Amesema kwa upande mwingine bado kuna kusuasua katika kugawa ardhi iliyofutiwa umiliki wake jambo linalokinzana na dhamira ya Rais Samia na linaloleta malamiko kutoka kwa jamii.
Amesema licha ya jitihada kubwa za serikali za kuimarisha sekta ya kilimo wakulima kwa ujumla bado wana changamoto nyingi za aina mbali mbali ya ardhi.
Amesema wakulima wadogo na wanavijiji kunyang’anywa ardhi zao bado ni kubwa na migorogo mingine ni ya muda mrefu na ni vigumu kuelewa ni kwa nini mpaka sasa haijapatiwa ufumbuzi.
Amesema changamoto ya bei za mazao na soko la uhakika kwa mazao ya wakulima bado ni kubwa na wana amini inafahamika vyema na pia changamoto ya mitaji na uwezeshaji kwa wakulima.
” Tunaamini kwamba njia rafiki lazima zitafutwe ili vyombo vya kifedha na programu za uwezeshaji ziweze kuwafikia wakulima wadogo,” amesema Ngorisa.
Mgeni rasmi wa mkutano huo wa 17 wa MVIWAMA, Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Manyara, Faraja Ngeragea amewataka wakulima kutumia vyema mvua hizi chache zinazonyesha kupanda mbegu mashambani mwao ili waweze kuvuna mazao.
Ngeragea amesema mvua za mwanzo ni za kupandia hivyo wakulima wanapaswa kupanda mbegu mashambani kwani watavuna mazao yao miezi michache ijayo.
“Wakulima wa Manyara wanapaswa kutumia vizuri mvua hizi chache kupanda mbegu zinazoendana na msimu huu kabla mvua hazijaisha,” amesema Ngeragea.
Amepongeza juhudi za MVIWAMA kusimamia wanachama zaidi ya 8000 kwa mkoa huo katika nyanja ya kilimo, ufugaji, mnyororo wa thamani wa nyuki, mbegu za asili na utunzaji wa mazingira.
“Kutokana na mabadiliko ya tabia nchi inabidi wakulima kujifunza mbinu za kilimo na ufugaji zinazokabiliana na mabadiliko haya tuliyonayo,” amesema Ngeragea.
Amehimiza wana MVIWAMA kutumia fursa zinazotolewa na Serikali ili kuboresha shughuli zao za kilimo na ufugaji zitakazokuwa na tija na kunufaika kiuchumi.