NA VICTOR MASANGU, KIBAHA
Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoa wa Pwani imeamua kuwapa motisha ya zawadi mbali mbali walipakodi bora baada ya kutambua juhudi na mchango wao mkubwa katika suala zima la kutii maagizo ya serikali katika ulipaji wa kodi.
Zawadi hizo zimetolewa na kamishina uchunguzi upande wa kodi Hashimu Ngodi aliyemwakilisha Kamishina Mkuu wa mamlaka hiyo ya TRA.
Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hizo zilizokwenda sambamba na kusikiliza changamoto za wawekezaji kiongozi huyo kutoka TRA amesema kuwa utaratibu huo utafanyika nchi nzima.
“Niko hapa namwakilisha kamishina tumeweka utaratibu wa kutoa zawadi kwa walipakodi bora na wakati huohuo tunasikiliza changamoto zinazowakabili ili tuzifanyie kazi”amesema
Ameongeza kuwa lengo la TRA ni kuona walipakodi wanalipa kodi kwa ari na moyo hali itakayowezesha serikaki kutoa huduma bora kwa jamii
Baadhi ya wawekezaji wamepongeza hatua hiyo na kueleza kuwa itaimarisha upendo na ushirikiano baina ya pande hizo mbili.
“Nashukuru kwa kutambuliwa na TRA nitaendelea kuwa mlipakodi mzuri na kuwa mfano wa kuigwa”amesema Velnatta Ramalah kutoka kiwanda cha Lake group Kibaha
Naye Emmanuel Amani amesema hatua ya TRA kuanza kuwatembelea walipa kodi na kusikiliza changamoto zao itajenga urafiki na imani kwao jambo litakalosaidia kuchochea maendeleo ya nchi kupitia mapato.