Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Shirikisho la Ethiopia zimesaini Hati sita (6) za Makubaliano ya Ushirikiano katika maeneo ya kimkakati ikiwemo: biashara, viwanda, mifugo, mafunzo ya anga, mafunzo ya utalii na masuala ya uhamiaji.
Makubaliano hayo yamesainiwa wakati wa Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Pamoja ya Mawaziri kati ya Tanzania na Ethiopia uliofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia tarehe 17 Desemba, 2024 chini ya uenyekiti wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia, Mhe. Dkt. Gedion Timothemas Hessebon.
Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Mawaziri ulilenga kujadili na kutathimini hatua za utekekelezaji zilizofikiwa katika masuala mbalimbali ya ushirikiano yaliyokubaliwa wakati wa uanzishaji wa tume hiyo mwaka 2017 pamoja na kuangalia maeneo mapya ya kimkakati ili kukuza ushirikiano uliopo.
Pamoja na masuala mengine mkutano huo umejadili na kukubaliana masuala mbalimbali ambayo ni: Umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano wa uwili katika siasa, diplomasia, ulinzi na usalama, masuala ya sheria na haki, biashara, kilimo, mifugo, utalii, nishati, maji, ujenzi wa miundombinu, usafirishaji, teknolojia ya Habari na mawasiliano, sayansi na teknolojia, afya, elimu, utamaduni, Sanaa na michezo.
Kuhusu Mkataba wa Ushirikiano wa Bonde la Mto Nile, Mawaziri hao wamesisitiza umuhimu wa usimamizi wa rasilimali maji na wamezipongeza nchi zilizosaini na kuridhia makubaliano hayo na kuzihimiwa nchi ambazo hazijakalimilisha kuchukua hatua za maksudi kukamilisha hilo kwa maslahi ya pande zote za ushirikiano.
Aidha, wamekubaliana kuongeza ushirikishaji wa sekta binafsi katika shughuli za kiuchumi ili kusaidia jitihada za Serikali kufikia malengo ya maendeleo endelevu. Ushirikishaji huo utaenda sambamba na utoaji hamasa kwa sekta binafsi kutumia fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta za ushirikiano na kuwajengea uwezo na ufahamu wa namna ya kuzifikia fursa husika.
Vilevile, wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika majukwaa ya kimataifa na kuonesha dhamira ya kuunga mkono jitihada za Umoja wa Afrika (AU) za kuyafikia malengo ya Agenga 2063 ambapo wameahidi kuendelea kufanya kazi pamoja ili kuimarisha mfumo wa amani na ulinzi wa AU.
Kwa pamoja Mawaziri hao wamewaelekeza wataalamu wa pande zote mbili kusimamia kwa tija makubaliano yaliyokubaliwa na kukamilisha Hati nyingine za Makubaliano ambazo zipo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji. Pia wamesisitiza umuhimu wa kuanzisha mfumo wa ufuatiliaji utekelezaji wa makubaliano yaliyokwisha sainiwa kwa kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara ili kuendelea kufungua maeneo mapya ya ushirikiano yenye tija kwa ustawi wa pande zote mbili.
Mkutano huo umehitimishwa kwa kusaini Tamko la Pamoja na kukubaliana kuwa Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Mawaziri utafanyika nchini Tanzania mwaka 2026 katika tarehe itakayokubaliwa na pande zote.