*RC Chalamila awataka kuibeba ajenda hiyo
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila amewaalika wananchi kushiriki kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia katika Wiki ya Nishati Safi ya Kupikia ya Rafiki Briquettes yenye kauli mbiu ya “Zima Mkaa wa Miti na Kuni, washa Rafiki Briquettes” iliyoandaliwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO)
Akiongea kuhusu kampeni hiyo kabambe inayotarajiwa kuanza Desemba 20 hadi 22, 2024 katika Mkoa wa Dar es Salaam, RC Chalamila amesema kwa kushirikiana na STAMICO wameandaa kampeni kabambe ambayo itahamasisha wananchi kutumia Nishati safi ya kupikia ambayo ni mkaa uliotengenezwa kwa teknolojia kubwa inayotumia malighafi ya Makaa ya mawe.
Amehamasisha wakazi wa Mkoa huo kujenga tabia ya matumizi ya Nishati Safi ya kupikia ambayo ndiyo dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa kinara Barani Afrika katika kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Ameitaka kampeni hiyo ya nishati safi ifanyike kwa ukubwa wake ili kuhakikisha wana Dar es Salaam wanapata uelewa na maarifa ya kutosha juu ya matumizi ya nishati hiyo hususani hatua zilizotumika kuifanya bidhaa hii kutokuwa na hewa hatarishi.
Aidha ametumia fursa hiyo kuwapongeza STAMICO kwa kuamua kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia jambo linalochukuliwa kama mkakati namba 1, katika jitihada za Serikali kuanza kupunguza matumizi ya mkaa utokanao na kuni.
“Niwapongeze STAMICO kwa kutengeneza bidhaa ambayo inaleta chachu ya kuhamasisha matumizi nishati safi ili kuondokana na nishati zenye athari kwa watumiaji.” Alisema RC Chalamila
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse amesema kampeni hii inayotarajiwa kuanza Desemba 20, 2024. hadi Desemba 22, 2024 ili kuweza kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi kwa wananchi.
Amesema Shirika limebuni teknolojia ya kutengeneza mkaa kwa kutumia malighafi ya makaa ya mawe ili kuunga mkono juhudi za Mhe Rais za matumizi ya Nishati safi ya kupikia kwa watanzania tena kwa bei nafuu ambayo kila mtanzania anaweza kuimudu hivyo amewataka watanzania kutumia fursa hiyo.
Ameongeza kuwa, kampeni itatoa nafasi ya kuwatambulisha mawakala wa mkoa wa Dar es Salaam, kutoa elimu ya matumizi sahihi ya Rafiki Briquettes ili waweze kuhama kutoka kwenye matumizi ya nishati zisizo safi na salama.