Naibu Waziri Kihenzile wakati akitoa maagizo kwa mkandarasi kufanya kazi usiku na mchana
Shughuli mbalimbali zikiendelea katika ujenzi wa jengo la abiria
Naibu waziri wa wizara ya uchukuzi David Kihenzile wakati akikagua uwanja wa ndege Sumbawanga
……………….
Neema Mtuka Sumbawanga
Rukwa ;Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi David Kihenzile amemtaka mkandarasi wa uwanja wa ndege wa mjini Sumbawanga kuongeza kasi ya utendaji kazi na kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.
Kihenzile amesema hayo wakati alipotembelea uwanja wa ndege wa Sumbawanga na kujionea hali halisi ya utendaji kazi inavyokwenda kwa kusuasua na kumtaka mkandarasi kufanya kazi usiku na mchana.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Desemba 17 mwaka huu Kihenzile amesema kuwa hajaridhiswa na kasi ya ujenzi wa uwanja huo ambao mpaka sasa ilibidi uwe na asilimia 65 lakini kwa kusuasua huku una asilimia 40.
“Namtaka mkandarasi afanye kazi mchana na usiku ili kuhakikisha anakwenda sambamba na makubaliano ya mkataba aliousaini na hakikisha unamaliza kwa wakati.”amefafanua Naibu waziri.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo Kaimu meneja wa Tanroads mkoa wa Rukwa Galasiano Tobagoze amesema kuwa zaidi ya sh Bill.60 zilitolewa kwa ajili ya ukarabati wa uwanja wa ndege wa sumbawanga.
Amesema ujenzi wa uwanja wa ndege umekamilika kwa asilimia 40 ambapo mkandarasi anaendelea na kazi ujenzi wa jengo la abiria na tabaka la juu yaani BBB ambao umefikia asilimia 46 na tabaka la chini CTB ambao umefikia asilimia 14.
Katika hatua nyingine Naibu waziri pia ametembelea bandari ya Kasanga na kujionea mabadiliko ya tabia nchi yalivyoathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za kimaendeleo ambazo zingeipatia serikali kipato kikubwa kupitia maghala yaliyopo katika bandari hiyo.
Amesema kuwa Bandari ya Kasanga iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo imekuwa ni chanzo kikuu cha mapato kwa kuingiza mizigo kutoka nchi jirani.
Aidha amesema kuwa serikali ya awamu ya sita imetenga fedha zaidi ya shilingi biliioni 600 ambapo sehemu ya fedha hizo itajengwa meli ya uukubwa wa tani elfu 3500 ambayo itafanya shughuli zake katika ziwa Tanganyika ikiwemo bandari ya Kasanga.
“Itakuwa meli ya kwanza kubwa na ya kisasa katika ziwa Tanganyika ,ziwa Victoria na ziwa Nyasa.”amefafanua
Naye Kaimu meneja wa Bandari ya kasanga mwambao wa ziwa Tanganyika Abdallah Yusufu Mohamed amesema wanapitia changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi ambapo maji yamesogea karibu na jengo la kukaa abiria.
Hata hivyo amesema wamejipanga kukabiliana na tatizo hilo kwa kuhakikisha wanatengeneza miundo mbiu ya hapo bandarini na kuendelea na shughuli za kimaendeleo bandarini hapo.
Baadhi ya wananchi wilayani Kalambo akiwemo Faudhia Juma amesema kukamilika kwa meli hiyo kutawanufaisha wakazi wa wilaya hiyo na kuchangia mapato kwa taifa.
Nao wafanyakazi wa uwanja wa ndege uliopo Sumbawanga Jabiri Salehe amesema wanapitia changamoto nyingi hasa mikataba mibovu inayomnufaisha mwajiri na kuwabana wao kwani hawapati stahiki zao kama inavyotakiwa.
“Mkataba unamtaka mwajiri nikifiwa kunilipa lakini wao hawafanyi hivyo na matokeo yake wanatufukuza kazi kwa kuonekana msumbufu jambo ambalo linakatisha tamaa na kurudisha nyuma maendeleo kwa wafanyakazi wazawa.”amefafanua
Amesema wao kama wafanyakazi wazawa hawajapewa kipaumbele na kufanya kazi na wengi kusimamishwa kwa sababu kama hizo ambazo ni kinyume na sheria na kuitaka serikali kuwatupia jicho ili kutatua changamoto inayowakabili.
Mradi huo wa ujenzi wa uwanja wa ndege unatarajiwa kukamilika Machi 2025 huku ukigharimu shilingi bilioni 60.