NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ametoa pongezi kwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi ikiwemo mradi wa ujenzi wa awamu ya tatu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), huku akitoa maagizo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya ujenzi Balozi Mhandisi Aisha Amour kuwasimamia wakandarasi wanaotekeleza mradi ya ujenzi ili kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana jambo ambalo litasaidia kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam.
Mradi wa ujenzi wa awamu ya tatu ya BRT kuanzia Mtaa wa Azikiwe Posta ya Zamani hadi Gongolamoto unaotekelezwa na Mkandarasi Sinohydron kwa gharama ya shilingi bilioni 230 na umefikia asilimia 70.
Akizungumza Disemba 15, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa awamu ya tatu ya BRT kuanzia Mtaa wa Azikiwe Posta ya Zamani hadi Gongolamoto na mradi wa uboreshaji wa barabara ya Morogoro kutoka Ubungo hadi Kimara, Waziri Ulenga amesema kuwa TANROADS wamekuwa wakifanya kazi vizuri.
Waziri Ulega amesema kuwa mradi wa ujenzi wa awamu ya tatu ya BRT kuanzia Mtaa wa Azikiwe Posta ya Zamani hadi Gongolamoto unatarajia kukamilia mwezi March 2025 na kuleta ahueni kwa wananchi.
“Mkandarasi atakayefanya vizuri tutampongeza pamoja na kumpatia kazi nyengine kadri ya sheria na utaraibu tutakavyo tuongoza, pa naomba wakazi wa Dar es Salaam kuwa wavumilivu katika kipindi chote ambapo ujenzi wa barabara unaendelea” amesema Waziri Ulega.
Akikagua mradi wa uboreshaji wa barabara ya Morogoro kutoka Ubungo hadi Kimara, Waziri Ulega amesema kuwa mkandarasi huyu yupo nyuma ya makubaliano ya utekelezaji wa mradi ambapo mpaka sasa amefikia asilimia 26 ya kazi yake badala ya asilimia 52 kama ilivyoainishwa kwenye mkataba.
“Mkandarasi amefanya uzembe, nimempa siku tatu kuhakikisha anaweka taa za barabarani ili kufanya kazi usiku na mchana, nitarudi usiku kukagua kama kweli wanatekeleza agizo hili” amesema Waziri Ulega.
Amesisitiza kuwa endapo mkandarasi atashindwa kutekeleza majukumu yake kwa wakati atachukuliwa hatua kali za kisheria pamoja na wahusika wote waliokuwa chini ya mamlaka yake.
Meneja wa mradi wa BRT – TANROADS Mhandisi Frank Mbilinyi, amesema kuwa wanaendelea na utekelezaji wa mradi awamu ya tatu wa BRT katika maeneo tofauti ikiwemo mradi uliopo Mtaa wa Azikiwe Posta ya Zamani hadi Gongolamboo ambao unatarajiwa kukamilika kwa wakati.
Mhandisi Mbilinyi amesema kuwa mradi mwengine ni Tegeta hadi mjini ambapo unatekelezwa kwa awamu tatu kutoka mjini hadi Mwenye, kutoka Mwenge hadi Ubungo, Mwenge hadi Tegeta.
“Kuna wakandarasi watatu ambao wapo katika hatua tofauti tofauti, mradi huo kwa mujibu wa mkataba unatakiwa kukamilika mwezi Aprili, 2025 tunaendelea kuwasimamia ili kuhakikasha wanafanya kazi usiku na mchana na kumaliza kwa muda uliopangwa” amesema Mhandisi Mbilinyi.