Dar es Salaam – Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry Slaa, ametoa wito kwa Bodi mpya ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kuhakikisha shirika hilo linaendeshwa kwa mtazamo wa kibiashara ili kuendana na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza leo, Desemba 16, 2024, wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo, Mhe. Slaa alimhimiza Mwenyekiti wa Bodi, David Nchimbi, kutengeneza mpango madhubuti wa kulibadilisha shirika na kuhakikisha linajiendesha kwa ufanisi wa kibiashara.
“Rais Samia alielekeza shirika hili lijiendeshe kibiashara. Hivyo, Mwenyekiti atengeneze mpango wa kuondoa changamoto zilizopo na kupeleka shirika kwenye ufanisi wa hali ya juu,” alisema Mhe. Slaa.
Waziri huyo aliongeza kuwa serikali imewekeza kiasi kikubwa cha fedha katika miundombinu ya mawasiliano, ikiwa ni pamoja na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Kituo cha Kitaifa cha Data. Aliitaka bodi kuhakikisha uwekezaji huo unaleta tija kwa taifa kwa kuongeza thamani ya huduma zinazotolewa na shirika.
“Shirika likiimarika linaweza kuchochea maendeleo katika sekta mbalimbali na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi,” aliongeza.
Mhe. Slaa alihimiza bodi kuchukua jukumu la kusimamia kwa umakini menejimenti ya shirika hilo na kuhakikisha uwajibikaji wa hali ya juu. “Uendeshaji wa shirika uko chini ya bodi. Wajumbe wote wa bodi simamieni vizuri menejimenti ili kufanikisha malengo tuliyojiwekea,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi, David Nchimbi, alimshukuru Rais Samia kwa kumteua na kuahidi kushirikiana na wajumbe wa bodi hiyo kuboresha utendaji wa TTCL. “Tutaleta mabadiliko makubwa na kupeleka shirika mbele kwa kasi,” alisema Nchimbi.
Bodi hiyo mpya inatarajiwa kusimamia mabadiliko ya TTCL kwa kuzingatia ufanisi wa kibiashara, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali za kuhakikisha sekta ya mawasiliano inachangia ipasavyo katika maendeleo ya taifa.