Kampuni ya Bakhresa kupitia kitengo chake cha Bakhresa Food Products Ltd leo imezindua rasmi bidhaa mpya ya juice inayojulikana kama African Fruit katika hoteli ya Hyatt Regency, Dar es Salaam. Uzinduzi huo ulihusisha nembo na vifungashio vipya vinavyoendana na lengo la kampuni hiyo la kuboresha muonekano wa bidhaa zake ili kushindana kimataifa na kuvutia masoko mapya.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Jafo, leo Desemba 16, 2024, akizindua rasmi nembo na vifungashio vipya vya juice ya African Fruit amewahimiza wakulima wa matunda nchini kuongeza juhudi katika uzalishaji wa mazao yao ili kufanikisha mahitaji ya viwanda vinavyotegemea malighafi za matunda.
Dkt. Jafo amewataka wakulima wadogo nchini kuchangamkia fursa za kilimo cha matunda, akisisitiza kuwa jitihada hizo zitachangia kwa kiasi kikubwa kulisha viwanda vya kuzalisha bidhaa za matunda.
“Ili kufanikisha maendeleo, tunahitaji uwekezaji mkubwa na wenye tija. Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia zaidi wawekezaji katika sekta mbalimbali,” alisema Dkt. Jafo.
Aidha, alilipongeza kundi la makampuni ya Bakhresa kwa kufanya uwekezaji mkubwa wa takriban Shilingi bilioni 700 katika mradi huo mpya, akisema kuwa ubunifu huo unaleta tija kwa kuongeza ushindani sokoni na kuboresha bidhaa.
Kwa mujibu wa Dkt. Jafo, bidhaa mpya za African Fruit zitatoa ajira kwa vijana, huku akibainisha kuwa mwaka 2022 kulikuwa na wahitimu wa shahada ya kwanza 51,000, idadi ambayo inatarajiwa kufikia 67,000 mwaka 2024.
“Serikali haiwezi kuajiri wahitimu wote. Sekta binafsi ni mhimili muhimu wa kutengeneza ajira kwa vijana, na eneo la viwanda limepewa kipaumbele kutokana na mchango wake mkubwa katika kupunguza changamoto za ajira,” aliongeza.
Uzinduzi huu ni sehemu ya juhudi za kuendeleza sekta ya viwanda nchini, hatua inayolenga kuboresha maisha ya Watanzania kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.