Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Utawala, Katiba na Sheria wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Florent Laurent Kyombo wamewasili nchini Ethiopia tarehe 15 Desemba 2024, kwa ziara ya kikazi ya siku 4 kuanzia tarehe 15 hadi 19 Desemba, 2024.
Baada ya kuwasili nchini humo, Kamati hiyo imepokelewa na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika (AU) na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Uchumi wa Afrika (UNECA), Mhe. Innocent Shiyo katika Ofisi za Ubalozi huo.
Lengo la ziara hiyo ni kujifunza, kupata uzoefu na kujenga uwezo juu ya usimamizi wa masuala ya Diaspora nchini Ethiopia ambapo, diaspora kwa sehemu kubwa wamekuwa wakichangia Maendeleo ya kiuchumi kwa nchi yao na kutengeneza fursa mbalimbali za ajira na kiuchumi kwa waethiopia.
Wabunge hao pia walipata nafasi ya kuonana na Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu waliopo nchini Ethiopia kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Pamoja ya Mawaziri (JMC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Shirikisho la Ethiopia utakaofanyika tarehe 17 Desemba, 2024.
Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu hao ni pamoja na, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, Katibu Mkuu Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Dkt. Aboud Suleiman Jumbe, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Abdul Mhinte na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Bw. Hussein Mohamed Omar.