Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita akikabidhiwa Kombe na Mkuu wa Kikosi Cha KVZ Meja Said Ali Shamuhuna huko Mtoni Wilaya ya Magharibi B, katika Sherehe ya kuipongeza Timu ya Netball ya KVZ (KVZ Queens) kufuatia kufanya vizuri katika Kombe la Muungano, lililofanyika Jijini Dar-es-salaam.
Mkuu wa Kikosi Cha KVZ Meja Said Ali Shamuhuna akizungumza na Maafisa na Wapiganaji wa kikosi Cha KVZ (hawapo pichani) katika Sherehe ya kuipongeza Timu ya Netball ya KVZ (KVZ Queens huko Mtoni Wilaya ya Magharibi A ambapo timu hiyo ilipata ushindi katika Kombe la Muungano lilifanyika Jijini Dar-es-salaam.
Mkuu wa Kikosi Cha KVZ Meja Said Ali Shamuhuna akimvisha cheo mmoja kati ya Wachezaji wa timu ya KVZ Queens huko Mtoni Wilaya ya Magharibi A ambapo Timu hiyo ilipata ushindi katika Kombe la Muungano lilifanyika Jijini Dar-es-salaam.
Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita akibadilishana mawazo na Mkuu wa Kikosi Cha KVZ Meja Said Ali Shamuhuna katika sherehe ya kuipongeza Timu ya KVZ Queens huko Mtoni Wilaya ya Magharibi A ambapo Timu hiyo ilipata ushindi katika Kombe la Muungano lilifanyika Jijini Dar-es-Salaam.
Katibu wa Michezo KVZ Captain Hassan Omar akitoa maelezo katika Sherehe ya kuipongeza Timu ya KVZ Queens kufuatia kupata ushindi katika mashindano ya Muungano yaliofanyika Jijini Dar-es-salaam, Sherehe ambazo zimefanyika Mtoni Wilaya ya Magharibi A.
Baadhi ya Washiriki na Wachezaji wa Timu ya KVZ Queens wakiwa katika sherehe ya kuipongeza Timu hiyo, kufuatia kupata ushindi katika mashindano ya Muungano yaliofanyika Jijini Dar-es-salaam, Sherehe zimefanyika Mtoni Wilaya ya MagharibiA.
……..
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita amesema Serikali inathamini Michezo yote na sio Mpira wa Miguu pekee.
Mhe. Tabia ameyasema hayo huko Mtoni KVZ, wakati wa Sherehe ya kuipongeza Timu ya Netball ya KVZ (KVZ Queens) kufuatia kufanya vizuri katika Kombe la Muungano, lililofanyika Jijini Dar-es-Salaam.
Amesema Serikali inaendelea kujenga Viwanja vya Michezo ili Wanamichezo waweze kushiriki michezo ya aina zote.
Aidha amesema, Wizara itaendelea kupanga mikakati ya kuhakikisha Timu hiyo na nyengine zinaendelea kushinda katika mashindano yanayofanyika ndani na nje ya Nchi ili kuipa hadhi Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Hata hivyo amewataka Wanamichezo wa Zanzibar kufanya mazoezi kwa bidii na kudumisha Nidhamu ili waweze kushinda mashindano yote yanayoandaliwa.
Mbali na hayo Mh. ameahidi kusaidia Vifaa mbalimba vya michezo ikiwemo Jezi, Mipira na Soksi ili kuunga mkono kazi kubwa inayofanywa na Timu hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi Cha KVZ Meja Said Ali Shamuhuna amesema kitendo cha Timu hiyo kuchukuwa Kombe hilo, ni kikubwa na kimetoa heshima kwa kikosi hicho na Taifa kwa ujumla.
Aidha amesema kwa upande wa Netball kwa sasa hawana wasiwasi sana, wanajiandaa zaidi na Mashindano ya Afika Mashariki yanayotarajiwa kufanyika Zanzibar lakini kwa sasa wanajipanga zaidi kwa Mchezo wa Mpira wa Miguu na Michezo mengine.
” Kwa upande wa Netball sisi ni Mabingwa wa Tanzania kwa vile tumeshinda Kombe la Muungano na sasa tunaelekeza nguvu zetu zaidi kwa Michezo mengine ikiwemo mpira wa Miguu”alisema Shamuhuna.
Nae Katibu wa Michezo KVZ Captain Hassan Omar amesema Timu hiyo, imefanikiwa kushinda mechi zote iliocheza na kutangazwa kuwa Bingwa wa Mashindano hayo mwaka 2024.
Mashindano hayo, yaliofanyika Jijini Dar-es-salaam, yamezishirikisha timu saba (7) tano kutoka Zanzibar na mbili (2) kutoka Dar-es-salaam ambapo Wachezaji wa Timu hiyo ambao ni wa kikosi cha KVZ wamepandishwa Vyeo na Wachezaji ambao ni Raia wamekabidhiwa fedha taslim.
Miongoni mwa timu saba (7) zilizoshiriki katika Kombe hilo kutoka Zanzibar ni pamoja na KVZ, Mafunzo, JKU, Zimamoto na Afya wakati kutoka Dar-es-saalam ni Uhamiaji na Magereza.
Imetolewa na Kitengo cha Habari, Mawasiliano na Uhusiano.