Happy Lazaro, Arusha .
Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU pamoja na watanzania kwa ujumla kuongeza jitihada katika mapambano dhidi ya Vitendo vya rushwa kwani bado rushwa ipo na inanyima haki za watanzania wengi.
Akifungua mkutano wa mwaka wa TAKUKURU jijini Arusha Makamu wa Rais aliyemuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, amesisitiza watumishi wa umma kuwa waadilifu kwani taarifa nyingi za maadili kwa Viongozi wa umma zimekuwa sio sahihi.
Ameitaka TAKUKURU kufuatilia nyaraka za mali kwa watumishi wa umma, kwani Kiongozi anapaswa kuwa mtu asiyetiliwa mashaka katika utekelezaji wa majukumu yake kwa umma, huku akiwataka Maafisa wa TAKUKURU kuwa Viongozi wa mfano katika maadili ya utumishi wa umma na kutoa taarifa za kweli za mali, madeni na jinsi yanavyopatikana kila mwaka.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Crispin Chalamila amesema ndani ya miezi 12 iliyopita Takukuru imeokoa fedha zaidi ya sh ,bilioni 18 kupitia operesheni mbalimbali za uchunguzi pamoja na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo na fedha hizo zilirejeshwa serikalini na nyingine kutumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kadiri ilivyokusudiwa na hivyo kuchangia katika ustawi wa wananchi.
Amesema program ya Takukuru Rafiki imelenga kutambua na kutafuta majawabu ya kero katika utoaji wa huduma, kero ambazo zikiachwa bila kutatuliwa zinaweza kusababisha vitendo vya rushwa kwani programu hiyo imekuwa yenye mafanikio makubwa kadiri ya mrejesho wa wananchi wanaopokea huduma na wadau wanaotoa huduma.
Amesema Taasisi hiyo imeendelea kuchunguza tuhuma za vitendo vya rushwa na pale penye ushahidi na kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) walifungua na kuendesha kesi mahakamani ambapo Jamhuri imeshinda kesi kwa asilimia 75.9 tofauti na mwaka jana ambapo jamhuri ilishinda kesi kwa asilimia 67.7 katika kesi zilizotolewa maamuzi.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu, amesema kipindi cha kuanzia mwaka 2022/2023 na 2024/2025 Takukuru iliajiri watumishi wapya 1,190 ikiwemo,magari mapya 195 yenye thamani ya sh, bilioni 39.174 ambayo yamesambazwa katika ofisi za TAKUKURU nchi nzima kulingana na mahitaji.
Pia majengo ya ofisi 23 yenye thamani ya jumla ya sh, bilioni 12.5 yamejengwa katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini,ikiwemo mikoa mitano ya Kilimanjaro, Simiyu, Iringa, Shinyanga, Morogoro naWilaya 18 Mvomero, Kongwa, Kilolo, Kiteto, Liwale. Momba Nyasa, Monduli, Kishapu, Rombo, Nzega, Nkasi, Kaliua, Rungwe, Mbulu, Ukerewe, Makete, Nyanghwale.
Amesema katika kuimarisha matumizi ya Teknolojia, Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Takukuru imetandaza mifumo na kununua vifaa vya TEHAMA kwa jumla ya bilioni 3. 443,pia katika kuboresha mazingira bora ya mahali pa kazi, wawezeshwa kupata samani za ofisi za gharama sh, bilioni 3.901.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtandao wa wabunge wa kupambana na rushwa Afrika,tawi la Tanzania(APAAC),cap George Mkuchika amesema wananchi bado wanaimani na takukuru na kuitaka Taasisi hiyo kutobweteka na baadhi ya mafanikio bali waendelee kutoa elimu na ukaguzi wa taarifa wanazotoa viongozi kuhusu umiliki wa mali zao.