Na. Mwandishi Wetu
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imesema uwepo wa mawakala kwenye vituo vya kuandikisha wapiga kura ni kielelezo cha uwazi kwenye zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya watendaji wa uboreshaji wa Daftari ngazi ya mkoa mkoani Mbeya, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele amesema pamoja na kuhakikisha zoezi linafanyika kwa uwazi mawakala pia watasaidia kuwatambua wananchi wanaoomba kuandikishwa.
“Wakati wa uboreshaji wa Daftari mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura. Jambo hili ni muhimu kwani litasaidia kuleta uwazi katika zoezi zima lakini pia mawakala hao watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika hivyo kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa za lazima,” amesema Jaji Mwambegele.
Ameongeza kuwa mawakala hao hawaruhusiwi kuwaingilia watendaji wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao vituoni.
Akizungumza wakati wa kufungua mkutano kama huo mkoani Iringa, Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Rufaa (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk amesema katika kuhakikisha zoezi hilo linakuwa la uwazi Tume imetoa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uboreshaji wa Daftari kwa asasi za kiraia 157 na asasi za kiraia 33 kwa ajili ya uangalizi wa zoezi hilo.
“Ni muhimu kutoa ushirikiano kwa asasi hizo zitakapofika kwenye maeneo yenu kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao. Tume itawapa vitambulisho kwa urahisi wa kuwatambua,” amesema Jaji Mbarouk.
Mafunzo hayo yanafanyika ikiwa ni maandalizi ya uboreshaji wa Daftari mkoani Mbeya, Iringa na mkoa wa Dodoma kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ambapo uboreshaji utafanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 27 Desemba, 2024 hadi tarehe 02 Januari, 2025 na vituo vitafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.