Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia Sayansi na Elimu ya Juu, Prof. Daniel Mushi, ametoa wito kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kusoma vitabu kama njia ya kuibua fursa za maendeleo na kuboresha maisha ya jamii.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa vitabu viwili vilivyoandikwa na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Mushi alisisitiza kuwa vitabu ni nyenzo muhimu kwa maendeleo ya sekta ya elimu na kilimo nchini. Ameipongeza SUA na waandishi wa vitabu hivyo kwa juhudi zao za kutafuta suluhisho kwa changamoto zinazowakabili wananchi.
“Tunapenda kuona wanataaluma wakijikita katika uandishi wa vitabu vinavyotokana na tafiti zao, ili kusaidia jamii kutatua changamoto mbalimbali na kuendana na mtaala mpya wa elimu unaolenga kukuza stadi za amali,” alisema Prof. Mushi.
Kwa upande wake, Rasi wa Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia ya SUA, Prof. Samwel Kabote, alisema vitabu hivyo vina uwezo wa kuboresha sekta ya kilimo na elimu endapo mawazo yaliyoandikwa yatafanyiwa kazi kwa vitendo, na hivyo kusaidia kupunguza umasikini.
Josephine Ng’ang’a, Mkurugenzi wa RECODA (Research, Community and Organizational Development Associates), alieleza kuwa moja ya vitabu hivyo, ambacho kinatumia mfumo wa RIPAT, kimekusudiwa kuwasaidia wakulima kutumia teknolojia za kisasa zilizothibitishwa ili kuongeza tija. Aidha, alisema vitabu hivyo vinaweza kutumika pia na watafiti na wadau wa maendeleo vijijini katika utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa jamii.
Dkt. Onesmo Nyinondi, mmoja wa waandishi wa vitabu hivyo na Mhadhiri Mwandamizi wa SUA, alibainisha kuwa changamoto ya wanafunzi kushindwa kuandika makala na majarida kwa umahiri ndiyo iliyomhamasisha kuandika kitabu chake. “Vitabu ni njia bora ya kuhamisha maarifa kwa wanafunzi, watafiti, na jamii kwa ujumla,” alisema Dkt. Nyinondi.
Uzinduzi huo uliofanyika katika kampasi ya Edward Moringe, SUA, mkoani Morogoro, ulihudhuriwa na wadau wa sekta ya kilimo na elimu wakiwemo viongozi wa SUA, watendaji wa serikali, na wawakilishi wa taasisi zisizo za kiserikali kama RECODA.
Vitabu hivyo vinatarajiwa kuchangia maendeleo endelevu kwa kuwapa wakulima, watafiti, na wadau wa elimu nyenzo za maarifa ya kuboresha maisha yao na jamii kwa ujumla.