Klabu ya Simba imeendelea kung’ara katika mashindano ya Kimataifa baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia katika mechi ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika iliyochezwa tarehe 15 Desemba, 2024, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jijini Dar es Salaam.
Mgeni rasmi wa mchezo huo alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari, aliyemuwakilisha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi. Akizungumza kabla ya mechi, Mhe. Johari aliishukuru klabu ya Simba kwa heshima ya kumualika na kuonyesha matumaini makubwa katika uwezo wa timu hiyo.
“Nina imani kubwa na timu yetu, na mara nyingi nikihudhuria michezo kama hii tunapata ushindi,” alisema Mhe. Johari huku akiwataka wachezaji wa Simba kuendelea kuwapa furaha mashabiki wa Tanzania.
Katika hotuba yake, pia aliipongeza klabu ya Yanga kwa kuonyesha ushindani wao barani Afrika kwa kutoka sare ugenini dhidi ya TP Mazembe huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ushindi wa Simba ulipokelewa kwa shangwe kubwa kutoka kwa mashabiki waliofurika uwanjani, huku Mwenyekiti wa klabu hiyo, Bw. Murtaza Mangungu, pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, wakimpongeza Mhe. Johari kwa kushiriki na kutoa hamasa kwa wachezaji na mashabiki.
Simba sasa inaendelea kuwa kielelezo cha mafanikio ya soka la Tanzania, ikiimarisha nafasi yake katika mashindano ya kimataifa huku ikiwapa mashabiki matumaini makubwa ya kuendelea kufanikisha malengo ya kushinda taji la Kombe la Shirikisho.