Naibu Waziri wa maji Kundo Mathew aliyetangulia, akipanda ngazi kwenda kukagua ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji linalojengwa katika mradi wa maji wa miji 28 katika manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,katikati katibu tawala wa wilaya ya Songea Mtela Mwampamba.
Meneja mradi wa kampuni ya China Civil Engineering Contruction Corpertion(CCECC)inayotekeleza mradi wa maji wa miji 28 katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma Han Peng kulia na Mhandisi Mshauri wa mradi huo Gowri Shankar,wakimsikiliza Naibu Waziri wa maji Mhandisi Kundo Mathew baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa mradi huo unaotekelezwa kwa gharama ya Sh.bilioni 145.
Naibu Waziri wa maji Mhandisi Kundo Mathew,akikagua ujenzi wa tenki la kuhifadhi lita milioni 2 za maji linalojengwa katika eneo la Chandamali kupitia mradi wa maji wa miji 28 katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
………………….
Na Mwandishi Maalum,
Songea
NAIBU Waziri wa maji Mhandisi Kundo Mathew,amekagua ujenzi wa mradi wa maji wa miji 28 ambao Serikali ya awamu ya sita imetenga Sh.bilioni 145 ili kupunguza changamoto ya uhaba wa maji kwa wakazi wa manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo Kundo alisema,ameridhishwa na ubora wa mradi huo wa maji unaotekelezwa na Kampuni ya CCECC kutoka China,lakini changamoto iliyopo ni kasi ya ndogo ya utekelezaji wake.
Naibu Waziri Kundo,amemtaka Mkandarasi kuhakikisha anaongeza nguvu kazi ya wafanyakazi hasa wanatoka ndani ya mkoa wa Ruvuma ili kuzalisha ajira za kutosha badala ya kuleta wafanyakazi kutoka maeneo mengine.
Aidha,amemuagiza kuweka mazingira rafiki kwa vibarua na wafanyakazi kwa kuwalipa kwa wakati ili wasisababishe migomo baridi inayoweza kusababisha ujenzi wa mradi huo kusimama na kutokamilika kwa wakati.
Naibu Waziri Kundo,amempongeza Mbunge wa Jimbo la Songea Dkt Damas Ndumbaro,kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuwasemea wananchi wa Jimbo hilo hatua iliyosaidia kuishawishi Serikali kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza mradi huo na miradi mingine ya maendeleo.
Akitoa taarifa ya mradi huo Mhandisi wa maji kutoka Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira manispaa ya Songea(Souwasa)Vicent Baimana alisema,hadi sasa Serikali kupitia wizara ya maji imeshamlipa mkandarasi fedha za malipo ya awali Sh.bilioni 21.87 kati ya Sh.bilioni 145.
Baimana alisema,mradi huo utahusisha ujenzi wa chanzo katika mto Njuga chenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 17 kwa siku,ujenzi wa mtambo wa kuchuja maji,matanki matatu yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 9.
Alitaja kazi nyingine zinazotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa bomba za kusambaza maji urefu wa kilometa 30.2,upanuzi wa mtandao wa bomba za kusambaza maji kilometa 34.7 katika manispaa ya Songea na ukarabati wa mtambo wa kuchuja na kutibu maji.
Kwa mujibu wa Boimana,kwa sasa mkandarasi anaendelea na ujenzi wa matenki matatu ambapo tenki la maji Milaya lenye uwezo wa kuhifadhi lita mlioni mbili limekamilika.
Aidha alisema,tenki la Chandamali ujenzi wake upo hatua ya utengenezaji wa mfuniko wa juu na tenki la Mahilo litkalokuwa na uwezo wa kuhifadhi lita milioni 5 lipo katika hatua za uchimbaji wa msingi na hadi sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 4.8.
Kwa upande wake katibu Tawala wa wilaya ya Songea Mtela Mwampamba,amempongeza Naibu Waziri Kundo kwa kufuatilia kwa karibu mradi huo na miradi mingine ya maji inayotekelezwa katika maeneo mblimbali hapa nchini.
Alisema,mradi huo ni mkubwa na utakapokamilika utakuwa suluhusho la upungufu wa mahitaji ya maji kwa wananchi wa Jimbo la Songea mjini na maeneo ya pembezoni mwa mji wa Songea ikiwemo kata ya Shule ya Tanga na kata nyingine za manispaa ya Songea.
Hata hivyo,ameiomba Serikali kupitia wizara ya maji kupanua mtandao wa maji kwenda vijiji jirani vya Jimbo la Peramiho hasa ikizingatia chanzo cha maji kitakachotumika katika mradi huo kinapatikana katika Mto Njuga uliopo katika Jimbo la Peramiho.