TAARIFA KWA UMMA
Kufuatia taarifa hii inayosambazwa katika Mitandao ya Kijamii, Jeshi la Polisi lingependa kutoa ufafanuzi kulingana na ushahidi uliokusanywa kupitia kwa watu mbalimbali na kupitia uchunguzi wa kisayansi uliokwisha fanyika hadi sasa.
Ni kweli kwamba taarifa za kupotea kwa Vincent Peter Massawe zilifikishwa Kituo cha Polisi Kigamboni tarehe 19.11.2024 na Mke wake na upelelezi ulianza mara moja na kuthibitisha kuwa ni kweli alikuwa na harusi tarehe 16.11.2024 na bàada ya harusi alitafuta gari yakuwarejesha ndugu zake na wageni wengine Moshi Mkoani Kilimanjaro.
Aidha, ushahidi mwingine uliopatikana ni kwamba wakati wa maandalizi aliazima gari kutoka kwa jamaa yake ili imsaidie katika shughuli za harusi yenye namba T.642 EGU aina ya Toyota Ractis.
Baada ya harusi hakurejesha gari hiyo kwa mwenyewe badala yake tarehe 18.11.2024 ambayo inadaiwa alikuwa anafuatiliwa na gari ambayo alikuwa anaitilia mashaka ndiyo siku hiyo hiyo aliuza gari hiyo kwa kiasi cha shilingi milioni tisa (9) akalipwa shilingi milioni nane ( 8) ikabaki milioni moja (1). Taarifa iliyopo inaonyesha kuwa siku hiyo hiyo alimtumia mke wake kiasi cha fedha ili alipe madeni mengine yaliyotokana na harusi ikiwepo coaster aliyokodisha kuwarejesha wageni wake Moshi.
Gari hilo aina ya Toyota Ractis limefuatiliwa na limekamtwa.
Aidha, ushahidi mwingine unaonyesha huyu Vincent Peter Massawe, pia anadaiwa na watu wengine wawili mmoja kiasi cha shilingi milioni hamsini na tatu (53) na mwingine shilingi milioni kumi na sita (16).
Ukweli wa tukio hili utafahamika muda si mrefu kama amejipoteza au la kulingana na mtiririko wa ushahidi ulivyo na hili linategemea hasa tukipata ukweli kutokà kwa mke wake kwani inadaiwa anao ufahamu mkubwa wa jambo hili. Mwisho Umma utajulishwa taarifa zilizo sahihi kuhusu Bwana Peter Vicent Masawe.
Imetolewa na:
David A. Misime – DCP
Msemaji wa Jeshi la Polisi
Makao Makuu ya Polisi
Dodoma, Tanzania