Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Mkuu wa Mkoa (SHIMIWI) wakiwa kwenye mkutano huo uliofanyika mkoani Mbeya kuanzia tarehe 12 hadi 13 Desemba, 2024.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Mkuu wa Mkoa (SHIMIWI), Bw. Alex Temba akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shirikisho hilo kwa wajumbe wa mkutano mkuu uliofanyika mkoani Mbeya kuanzia tarehe 12 hadi 13 Desemba, 2024.
Katibu Mkuu Mstaafu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Bw. Mohamed Kiganja (mwenye kofia), akifuatilia mambo mbalimbali kwenye Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Mkuu wa Mkoa (SHIMIWI) uliofanyika mkoani Mbeya kuanzia tarehe 12 hadi 13 Desemba, 2024 mkoani Mbeya.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Emmanuel Kayuni akifungua mkutano mkuu wa Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali, na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI), uliofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 12 hadi 13 Desemba, 2024 mkoani Mbeya.
……….
Na Mwandishi Wetu, Mbeya
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI), wamehimizwa kulinda mafanikio waliyopata kwa kuendelea kuendesha michezo hiyo kwa ufanisi na utamaduni wa Mtanzania.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Emmanuel Kayuni wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa Shirikisho hilo uliofanyika tarehe 12 Desemba, 2024 mkoani Mbeya, ambapo amesisitiza wajumbe waendelee kusimamia michezo hii kwa kuzingatia katiba, sheria na kanuni, ili kuwawezesha watumishi kushiriki vyema kwenye michezo hii.
Bw. Kayuni amesema pamoja na changamoto zilizojitokeza kwenye michezo iliyopita bado wajumbe ambao ni viongozi wa klabu zinazoshiriki kwenye michezo hiyo, wanakila sababu ya kuhamasisha wanachama wenzao wanaosuasua kushiriki kwenye michezo kuhakikisha wanashiriki, ili kuleta tija na mafanikio mahala pa kazi.
“Ni jambo la kushukuru sisi tuna mashindano kila mwaka kwani hapa tumemsikia Mwenyekiti akisema sisi Tanzania tuna utaratibu mzuri, kwani majirani zetu hawana hii michezo ya watumishi, tunamshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt, Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu watumishi kushiriki michezo hii kila mwaka,” amesema Bw. Kayuni
Hata hivyo, amewakumbusha wachezaji kupima afya zao kabla ya kushiriki kwenye michezo ili kujiepusha na matatizo ya kiafya wanayoweza kuyapata.
“Kuna kipindi nilikuwa namsikiliza Profesa Janabi anasema kabla ya kuanza mazoezi lazima tupime afya, hivyo tusisahau kupima afya zetu,” amesema Bw. Kayuni.
Halikadhalika, amewaomba wajumbe wa mkutano wa SHIMIWI kuupa nafasi kwa mara nyingine tena mkoa wa Mbeya kuandaa michezo ya mwakani 2025, kwa kuwa wenyeji wake ni wakarimu, kuna malazi na vyakula vya kutosha, na ameahidi wataboresha miundombinu.
Naye Mwenyekiti wa SHIMIWI, Bw. Daniel Mwalusamba amesema suala hili la michezo linahadithi ndefu ya mafanikio ambapo wapo watu walioweza kuboresha afya zao kwa kufanya mazoezi, hivyo amewahimiza watumishi wa umma wote kufanya mazoezi mahala pa kazi na wasisubiri kipindi cha michezo pekee, kwani watumishi wenye afya njema hufanya kazi kwa ufanisi katika ujenzi wa taifa
Bw. Mwalusamba amesema viongozi wa klabu waandae ratiba na program za kuwakutanisha kwenye mazoezi mahala pa kazi na kuandaa pia mabonanza ambayo watapanga shughuli mbalimbali za kufanya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa RAS Mara, Bw. Ahidi Jairo amesema mkutano huu wa mwaka ni muhimu, kwani unatoa fursa ya kujitathmini kwa matukio yaliyofanyika kwa mwaka mzima katika michezo, ambayo inalengo pia la kujenga mahusiano ya kikazi baina ya mtumishi mmoja na mwingine wanaotoka maeneo mbalimbali ya kazi, na huleta nidhamu
“Hii mikutano inatija kubwa sana na inasaidia sana kutambua wapi tumekosea au tumefanya vema ili tuzidishe ubora, na hata kuja kwenye michezo au mkutano ni sawa na umeweka akiba kwani kwa watumishi wa umma hawawezi kujua kesho yao, na huenda ukahamishwa mkoa mmoja kwenda mwingine na ukakutana na wanamichezo, inajenga undugu na urafiki katika kuendeleza gurudumu la maendeleo” amesema Bw. Jairo.
Naye Katibu Mkuu wa RAS Mbeya, Bi. Liliani Gombanila amesema michezo husaidia kujenga afya ya mwili, akili, utendaji wa kazi unaongeza na magonjwa kupungua.