Na Sophia Kingimali.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Jenifa Omolo amesema TAASISI ya Uhasibu Tanzania(TIA) ni miongoni mwa taasisi zilizowezeshwa jumla ya shilingi za Kitanzania Bilioni 58.1, kwa ajili ya kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo hususan ujenzi wa miundombinu ya kusomea na kufundishia.
Pia ameipongeza Taasisi hiyo kwa kuwa mstari wa mbele kupitia mpango wa vituo atamizi, unaowawezesha wanafunzi kujiajiri, kuajirika, na kuchangia uchumi wa taifa.
Pongezi hizo amezimetowa leo Desemba 13, 2024 wakati akimwakilisha Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba katika Mahafali ya 22 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) katika Kampasi ya Dar es Salaam.
Aidha, amewapongeza kwa kuwaendeleza wanafunzi wenye mawazo ya kibunifu ili waweze kufanikisha malengo yao.
Amesema katika ulimwengu wa sasa wa teknolojia, amewasihi wahitimu kutumia ubunifu wao kutatua changamoto na fursa za kijamii.
“Mitandao ya kijamii ni rasilimali yenye nguvu. Itumieni kwa njia chanya kama vile kujifunza, kujitangaza kibiashara, na kujipatia kipato”. Amesema.
Aidha ameutaka uongozi na watumishi wa TIA kuhakikisha miradi hii inatekelezwa kwa wakati huku akiwasisitiza kuhakikisha wanaweka mipango Madhubuti ya kutunza miundombinu hiyo.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA Prof.William Pallangyo amesema jumla wahitimu 6,950 wametunukiwa katika ngazi mbalimbali ambapo kati ya wahitimu hao wanawake ni 3,838 na wanaume 3.112.
Aidha Prof.Pallangyo ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia jumla ya shilingi bilioni 58.1 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara Profesa Jehovaness Aikael ameipongeza Serikali kwa juhudi zake kubwa katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kupitia ujenzi wa miundombinu katika Kampasi zake za Mbeya, Mtwara, Mwanza, Singida na Zanzibar.
Pia amewaka wahitimu hao kuwa mabalozi wazuri wa TIA kwa kuonesha uadilifu na ufanisi. “Peperusheni bendera ya TIA kwa mafanikio, na endeleeni kuwa mfano wa kuigwa katika jamii na sehemu za kazi”.Amesema.