Na Mwandishi wetu, Mirerani
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Kituo cha Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, imetoa msaada wa vyakula kwa ajili ya kusaidia kituo cha watoto yatima na wenye uhitaji maalum wa Light In Africa.
Mkuu wa TAKUKURU Mirerani, Sultan Ng’aladzi akizungumza wakati wa kukabidhi misaada hiyo ya unga, sukari, mafuta ya kupikia na pipi amesema wafanyakazi wa kituo hicho wamejitoa ili kusaidia kituo hicho.
Ng’aladzi amesema wafanyakazi wa kituo cha Mirerani wamejitoa binafsi fedha zao na kununua mahitaji hayo mbalimbali kwa lengo la kuwasaidia watoto hao.
Ametoa wito kwa jamii, mashirika, taasisi za serikali na binafsi kujitoa ili kusaidia watoto hao wenye uhitaji mbalimbali waweze kupata faraja wakiendelea kulelewa kituoni hapo.
“Watoto hawa ni wetu sote hivyo jamii, mashirika na taasisi mbalimbali tujitoe kwa moyo mmoja ili kuwapa nguvu watoto hawa ambao wapo katika kituo hiki cha Light In Africa,” amesema.
Mmoja kati ya wasimamizi wa kituo hicho Mariam Mkali amesema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa usafiri wa uhakika.
“Hatuna usafiri na hata inapotokea mmepata mgonjwa ghafla mnashindwa kumpakia hata kwenye pikipiki mtoto mwingine hivyo tungepata usafiri ingekuwa vyema kwetu,” amesema.
Amesema pia eneo walilopo ni dogo kwa kutoa huduma kwa watoto hao hivyo wangepata eneo kubwa wangefurahi tofauti na sasa mahali walipo.
Hata hivyo, wamewapongeza viongozi wa Serikali hususani kituo cha afya Mirerani kwa kutoa kipaumbele kwa watoto wa kituo hicho kwani wakipata changamoto ya maradhi wanatibiwa vyema.